Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kuzingatia sheria, kanuni za nchi kabla ya kuwasilisha kero zao kwa viongozi mbalimbali ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kiurahisi.
Mhe. Mtambi ametoa kauli hiyo baada ya kupokea kero ya baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Musoma ambao wanaituhumu Halmashauri ya Manispaa ya Musoma kuvamia maeneo yao na kujenga Shule za Kata bila kufanya mazungumzo wala makubaliano nao kuhusu hatma ya maeneo yao.
“Mimi kama Mkuu wa Mkoa sipindishi sheria wala situngi sheria mpya, haiwezekani ukavamiwa kama mnavyosema na kwa miaka 17 sasa huwajawahi kwenda Baraza la Ardhi la Kata, Baraza la Ardhi Wilaya wala Mahakamani ambavyo ndiyo vyombo vya kisheria kwa ajili ya kupata haki” amesema Mhe. Mtambi
Mhe. Mtambi baada ya kusikiliza pando zote mbili amewaelekeza wananchi hao kwenda kufungua kesi Baraza la Ardhi la Kata na kuwasilisha vielelezo vyao kama wanaushahidi wa maeneo hayo kuvamiwa bila makubaliano na Halmashauri ili waweze kuipata haki yao.
Mhe. Mtambi amesema ofisi yake itapokea mamalamiko ambayo yamefuata taratibu za kisheria lakini haki haijatendeka sehemu mbalimbali ikiwemo mahakamani au katika mabaraza ya ardhi ya Kata na Wilaya ili kuangalia uwezekano wa kusaidia wananchi kupata haki yao.
Aidha, Mhe. Mtambi amebadilisha maamuzi aliyoyatoa kuhusu eneo la Kijiji cha Bumangi, Wilaya ya Butiama baada ya kugundua kuwa katika maelezo ya viongozi wa Kijiji hawakusema kuwa Mahakama iliamua kuwa ardhi iliyokuwa inagombewa ni mali ya familia ya Mzee Mseti na hivyo kugawiwa kwenye shauri la ndoa ilikuwa ni halali.
Kanali Mtambi ametoa maamuzi hayo baada ya kubaini kuwa Serikali ya Kijiji cha Bumangi hawakuwa na uthibitisho kuwa eneo hilo ni mali halali ya kijiji hicho na kwamba alipewa Mzee Mseti kwa muda na wakati wa kesi ya talaka liligawiwa kama mali za wanandoa hao na kuwataka viongozi hao wakae na Mwanansheria wa Serekali kuona kama wanavigezo vya kufungua kesi mahakamani kudai eneo hilo.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara ametoa siku saba kwa uongozi wa Kijiji cha Butiama kujadili na kutoa fidia ya ardhi kwa familia moja iliyotoa ekari 17 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia, Butiama.
Mhe. Mtambi ametoa maamuzi hayo baada ya kijana mmoja wa familia hiyo kuleta shauri hilo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huku ndugu yake akipeleka shauri hilo kwa wanasheria kutaka kufungua kesi mahakamani kudai ardhi ya familia yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma Bwana Bosco Ndunguru aliyeshiriki sehemu ya vikao hivyo amesema Halmashauri haijawahi kupokea rasmi malalamiko ya wananchi wa Manispaa ya Musoma wanaolalamikia kuvamiwa katika maeneo yao na kujenga shule za kata.
Bwana Ndunguru ameeleza kuwa taarifa rasmi zilizopo katika ofisi yake ni kuwa wakati wanajenga shule za Kata katika maeneo yanayolalamikiwa, wananchi waliokuwepo walitoa maeneo kwa hiari na ndio maana pamoja na kuwa wanadai walivamiwa katika kipindi chote hicho hawajawahi kuwasilisha madai yao rasmi wala kwenda kwenye vyombo vya kisheria.
Katika shauri hilo pia ilibainika baadhi ya walalamikaji waliokuwa wanafuatilia hawakuwa na maeneo katika shule hizo na walipohojiwa walisema wao wanawasaidia walalamikaji wanaodai kuvamiwa katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Musoma Mhe. William Gumbo ameeleza kuwa alikuwepo katika kamati ya ujenzi wa shule za kata 13 katika miaka ya 2006 hadi 2010 akiwa mmoja ya wajumbe waliozunguka kutafuta fedha za ujenzi.
Mhe. Gumbo anasema maeneo hayo yalitolewa na wananchi kwa hiari na hapakuwa na mgogoro wowote ule wakati wa ujenzi mpaka wanamaliza na mgogoro umekuja kuibuka miaka ya hivi karibuni baada ya baadhi ya watu kujitokeza kuanza kudai fidia.
“Ninakumbuka kulikuwa na kiwanja kimoja kilikuwa na mgogoro kwa wakati huo na tayari Halmashauri iliweka viashiria vya ujenzi katika uwanja huo na baada ya mgogoro waliliacha eneo hilo na kwenda kujenga katika uwanja mwingine” amesema Mhe. Gumbo.
Mhe. Gumbo amesema amekuwa Diwani kwa muda mrefu na baadaye Meya wa Manispaa ya Musoma tangu mwaka 2015 hajawahi kupokea malalamiko rasmi kutoka kwa walalamikaji kuwa maeneo yao yalivamiwa lakini anachoelewa maeneo hayo yalichukuliwa kwa maridhiano na baadhi ya wananchi hao walilipwa fidia.
Katika kusikiliza malalamiko na kero za wananchi Mkuu wa Mkoa alikuwa pamoja na Kamati ya kusikiliza malalamiko na baadhi ya maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Halmashauri za Butiama na Manispaa ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa