Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 13 Agosti, 2024 amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na kuiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kukamilisha bweni lililojengwa kwa michango ya wananchi na wanafunzi waliomaliza Shule ya Sekondari Ngoreme ili wanafunzi wa kidato cha tano wapate sehemu stahiki ya kulala.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya shule hiyo, Mhe. Mtambi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Dkt. Maulid Suleiman Madeni kutumia fedha za mapato ya ndani kukamilisha ujenzi wa bweni hilo haraka iwezekanavyo.
“Ninatoa wiki sita bweni hili lililojengwa kwa nguvu za wananchi liwe limekamilika na wanafunzi wanaolala madarasani wawe wamehamia katika bweni hili na nipate taarifa ya utekelezaji wake” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ameitaka Halmashauri hiyo kusimamia ujenzi wa mradi wa mabweni mengine mawili, matundu nane ya vyoo na madarasa matano uliofadhiliwa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick wenye gharama ya shilingi 401, 800,000 ili uweze kukamilika kwa mujibu wa mkataba wake na kwa ubora unaotakiwa.
Kanali Mtambi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kupima matofali yanayotumika katika ujenzi wa mradi huo ili kujiridhisha kitaalamu kuhusu ubora wa tofali hizo na kuwasimamia mafundi kwa karibu katika mradi huo ili watekeleze mradi huo kwa mujibu wa utaratibu za ujenzi.
Aidha, Kanali Mtambi amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Serengeti kuisimamia Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na kuhakikisha inatekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi kwa kutumia mapato ya ndani na kufuta historia ya kutokutekeleza miradi ya wananchi iliyokuwepo katika Halmashauri hiyo.
Mhe. Mtambi amewapongeza wananchi wa eneo hilo kwa kuchangia ujenzi wa bweni hilo pamoja na miundombinu mingine ya huduma za jamii katika eneo hilo ili kujiletea maendeleo yao.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Shule ya Sekondari Ngoreme Bwana Daniel Mgaya Mwita amesema bweni hilo lilijengwa kutokana na michango ya wananchi na wanafunzi waliomaliza katika shule hiyo kwa gharama ya shilingi milioni 78 hadi hatua iliyofikia.
Mwalimu Mwita amesema kuwa jengo hilo lililopo kwenye hatua ya ukamilishaji na liliwekewa jiwe la msingi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2017 na Halmashauri iliahidi kukamilisha jengo hilo jambo ambalo halijafanyika na kusababisha wanafunzi wa kidato cha tano kulala katika madarasa yaliyogeuzwa kuwa mabweni katika shule hiyo.
“Ili kukamilisha bweni hilo na wanafunzi waweze kulitumia inahitajika shilingi milioni 30 kwa ajili ya vifaa na fedha za kuwalipa mafundi watakaofanya ukamilishaji wa mradi huo” amesema Mwalimu Mwita.
Mwalimu Mwita amesema shule hiyo kwa sasa ina wanafunzi 791 wa kidato cha kwanza hadi cha nne wanaosoma kutwa na mwaka huu imepokea wanafunzi 73 wa kidato cha tano ambao wanasoma bweni kati ya wanafunzi 91 waliopangiwa kusoma katika shule hiyo.
Aidha, Bwana Mwita amesema ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita, shule hiyo imepokea fedha katika mradi wa miundombinu ya kidato cha tano awamu ya pili iliyotolewa na Mgodi wa Barrick na ujenzi wa miundombinu hiyo unaendelea.
Bwana Mwita amezitaja changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa mradi huo mpya kuwa ni pamoja na kukosekana kwa tofali katika eneo hilo na kulazimika kuzifyatua katika eneo la mradi na changamoto ya maji kutokana na uhaba wa maji katika bomba la kijiji hicho jambo ambalo linasababisha mradi huo kupata maji kwa mgao jambo ambalo linachelewesha ukamilishaji wa mradi huo.
Ziara hiyo imehudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama wa Wilaya ya Serengeti, Mbunge wa Serengeti, baadhi ya maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, taasisi za umma, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa