Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 21 Julai, 2025 amefanya ziara katika Wilaya ya Serengeti na kukagua Mradi wa Maji wa Miji 28 katika Mji wa Mugumu na kumtaka mkandarasi Mega Engineering and Infrastructure Company Limited kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Mhe. Mtambi amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa mkandarasi ikiwemo kutoa fedha za kutekeleza mradi huo kwa wakati, hivyo hakuna sababu ya msingi kwa mkandarasi kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo.
“Mradi huu ulipaswa kukamilika mwezi Aprili, 2025 na ukaomba kuongezewa muda hadi Desemba, 2025 ninaomba ujue kuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza baada ya hapo, mradi huu ukamilike kwa wakati” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema kwa sasa mkandarasi hana madai ambayo hayajalipwa na vifaa vyote vipo katika eneo la mradi na kuwataka wasimamizi wa mradi huo pamoja na mkandarasi kushirikiana na kukamilisha mradi kwa wakati ili wananchi waweze kupata maji safi na salama.
Aidha, Kanali Mtambi ameonyesha kufurahishwa na maendeleo ya mradi huo na kumpongeza mkandarasi kwa kazi zinazoendelea baada ya kuongezewa muda wa utekelezaji wa mradi huo na kumtahadharisha kuwa Serikali haitatoa muda mwingine wa nyongeza katika mradi huo.
Akizungumza kuhusiana na mradi huo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) Mhandisi Nicas Mugisha amesema mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 21 ulianza kutekelezwa mwezi Aprili, 2023 na unatarajiwa kukamilika Desemba, 2025.
Mhandisi Mugisha amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuondoa adha ya maji kwa watu zaidi ya laki moja wa Mji wa Mugumu katika Wilaya ya Serengeti.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa ameiongoza Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara kukagua miradi itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 katika Wilaya ya Serengeti.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa ameambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Kamati ya wataalamu ya Mkoa, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti na wataalamu mbalimbali kutoka MUWASA na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa