Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo ameongoza hafla ya kuwapongeza walimu waliohusika na matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka 2024 iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Songe, Manispaa ya Musoma na kuwaahidi kuwapa gari walimu wataoaofanya vizuri kwenye mtihani wa mwaka 2025.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mtambi amesema mwakani zawadi zitaboreshwa na kutakuwa na zawadi ya Mkoa yeye atawatafutia walimu watakaokuwa wamefanya vizuri zawadi ya gari ili kuwapa motisha katika utendaji wao.
“Mwakani ofisi yangu itaboresha zawadi kwa walimu na shule zitakazofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka walimu kuondoa ufaulu wa daraja la tatu katika matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka 2025 na kuongeza ufaulu kidato cha pili na cha nne kwa shule zote za Sekondari za Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi amewapongeza walimu waliofanikisha ufaulu wa asilimia 100 katika matokeo hayo kwa kazi kubwa walioifanya na kuongeza kuwa Serikali na wananchi wa Mkoa wa Mara wanatambua kazi hiyo na umuhimu wake katika maendeleo ya nchi yetu.
“Nitoe wito kwa walimu na wasimamizi wa elimu katika Mkoa wa Mara kuendelea kuhakikisha matokeo haya yanaendelea kuboreshwa ili Mkoa sio tu ufaulishe kwa asilimia 100 bali wanafunzi wapate ufaulu mzuri utakaowawezesha kwenda vyuo vikuu” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewaahidi walimu kuwa Serikali inaendelea kushughulikia stahili zao kwa kadiri inavyopokea na kuwataka wasimamizi wa elimu katika nafasi mbalimbali kusimamia ufundishaji na ujifunzaji ili kuboresha ufaulu wa wanafunzi.
Mhe. Mtambi amewataka walimu kusimamia maadili na nidhamu ya wanafunzi wawapo shuleni ili wanapomaliza pamoja na ufaulu wawe wamepata malezi mazuri yatakayowasiaidia katika maisha yao ya baadae.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka akizungumza katika hafla hiyo amewapongeza walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwaahidi ushirikiano kutoka kwa Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Ofisi zetu Wakuu wa Wilaya zipo wazi kama kuna jambo lolote msisite kutushirikisha ili tulifanyie kazi kwa pamoja kulitatua” amesema Mhe. Chikoka.
Mhe. Chikoka amewapongeza walimu kwa kufuta ufaulu wa daraja sifuri na daraja la nne katika matokeo hayo na kuwataka kuhakikisha kuwa katika matokeo ya mwakani Mkoa unafuta ufaulu wa daraja la tatu.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Dkt. Zabron Masatu, amesema katika mtihani huo jumla ya shule 28 zenye wanafunzi 3,559 waliosajiriwa kufanya mtihani huo ambapo wanafunzi 20 hawakufanya kutokana na sababu mbalimbali huku wanafunzi 3,539 waliofanya wakifaulu kwa asilimia 100.
Dkt. Masatu amesema ufaulu huu wa asilimia 100 ni mwendelezo wa ufaulu ambapo katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2023 wanafunzi wote walifaulu huku mmoja tu akiwa amepata daraja la nne na wengine wakipata madaraja ya kwanza, pili na la tatu.
Dkt. Masatu ameipongeza Shule ya Sekondari ya Tarime kwa kuongoza kitaifa kuwa na wanafunzi wengi waliopata daraja la kwanza aidha amezipongeza shule 10 ambazo zimefaulisha kwa daraja la kwanza na la pili tu katika matokeo hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule Natta Sekondari, Mwalimu Mwema Machage amesema katika shule hiyo matokeo ya mtihani wa kidato cha sita wanafunzi 128 walipata daraja la kwanza na wanafunzi nane walipata daraja la pili.
Mwalimu Machage amesema matokeo ni suala jumuishi kati ya wasimamizi wa elimu, walimu na wanafunzi na katika shule hiyo wanafunzi wakianza kidato cha tano wanatakiwa kusema malengo yao katika maisha na shule inawapatia mkataba wa kitaaluma na mara kwa mara wanafunzi wanawakumbushwa kuhusiana na utekelezaji wa mkataba huo.
“Sisi tunawapokea wanafunzi wenye ufaulu wa kawaida kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu kama zilizvyo shule nyingine na shule pia inaweka malengo na wanafunzi na walimu ili kuhakikisha wote wanatimiza wajibu wao” amesema Mwalimu Machage.
Mwalimu Machage amesema kwa mwaka huu Shule hiyo iliweka lengo la wanafunzi wote wapate ufaulu wa daraja la kwanza hata hivyo nane walipata ufaulu wa daraja la pili na kwa mwakani malengo yao ni wanafunzi wote wapate daraja la kwanza na mwisho iwe pointi saba na wanaendelea kufanyia kazi malengo haya.
Shule tatu bora zilizopewa zawadi ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Natta (Serengeti), Shule ya Sekondari ya Bunda na Shule ya Sekondari ya Songe huku Shule ya Sekondari ya Tarime ikipewa zawadi kwa kutoa wanafunzi wengi wenye ufaulu wa Daraja la Kwanza.
Shule zilizozawaidiwa kutokana na ufaulu wa masomo ni Natta Sekondari somo la General Studies, Tarime Sekondari somo la Historia, Nyamunga Sekondari somo la Jiographia, Bunda Sekondari masomo ya kiingereza na uchumi na Bumangi Sekondari masomo ya Kiswahili, Biolojia, Basic Applied Mathematics, na Kemia,
Shule nyingine zilizozawadiwa ni Butuli Sekondari somo la Fizikia, Kowaki Girls somo la
Advanced Mathematics, Makongoro Sekondari masomo ya Biashara na Uhasibu na Ikizu Sekondari somo la Divinity.
Aidha, shule 10 zimetambuliwa kwa kupata ufaulu wa daraja la kwanza na la pili pekee wakati Wakuu wa Shule zote 28 wametambuliwa kwa kutunukiwa vyeti kufaulisha kwa asilimia 100.
Halfla hiyo ilihudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wenyeviti na wakurugenzi wa Halmashauri zote, Wakuu wa Shule za Sekondari na walimu waliohusika katika kufanikisha matokeo hayo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa