Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo amewapongeza walimu na wanafunzi waliohitimu kidato cha sita mwaka 2023 katika Mkoa wa Mara kwa kufanikisha ufaulu wa wanafunzi kwa asilimia 100.
Mhe. Mtanda ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake kuhusiana na matokeo ya kidato cha sita mwaka 2023 yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) hivi karibuni.
“Ninawapongeza sana walimu, wanafunzi, wasimamizi wa sekta ya elimu na wale wote waliohusika kwa kufanikisha wanafunzi wote 3091 waliofanya mtihani huo kufaulu na Mkoa kupata ufaulu wa asilimia 100” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa ufaulu wa Mkoa wa Mara umepanda kwa asilimia 0.9 kutoka ufaulu wa asilimia 99.1 kwa mtihani wa kidato cha sita mwaka 2022.
Aidha Mhe. Mtanda ameipongeza Shule ya Sekondari ya Tarime iliyopo katika Mji wa Tarime ambayo watahiniwa wake 357 kati ya 498 waliofanya mtihani katika shule hiyo mefaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza, 130 wamefaulu kwa daraja la pili na watahiniwa 11 wakiwa wamepata daraja la tatu.
“Shule hii imeongoza Kitaifa kuwa na wanafunzi wengi wa shule moja waliopata ufaulu wa daraja la kwanza katika tahasusi mbalimbali” amesema Mhe. Mtanda.
Aidha, amezipongeza Shule za Sekondari za Natta na Bunda kwa kuingia katika kumi bora kitaifa kwenye makundi yao katika matokeo ya mtihani huo.
Katika mtihani wa Taifa wa kidato cha sita mwaka 2023, wanafunzi 3,106 walidahiriwa kufanya mtihani wa kidato cha sita katika Mkoa wa Mara, wanafunzi 3091 walifanya mtihani na wanafunzi 15 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa