RC AMPONGEZA MWEKEZAJI MARA MINING INVESTMENT
Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo ametembelea Mgodi wa Dhahabu wa Mara Miningi Investment katika Kijiji cha Kerende, eneo la Nyamongo katika Wilaya ya Tarime na kumpongeza mmiliki wa mgodi huo kwa kufanya uwekezaji mkubwa.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua migodi katika mgodi huo, Mheshimiwa Mzee amempongeza mmiliki wa mgodi huo kwa uthubutu katika uwekezaji.
“Ninakupongeza sana kwa uwekezaji unaoufanya na kuweza kutoa kodi kwa serikali na ajira kwa watanzania na maendeleo katika eneo hili” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, akiwa katika eneo hilo Mkuu wa Mkoa alipokea taarifa za maendeleo ya mgodi huo na kukagua shughuli za mgodi.
Akitoa taarifa ya mgodi huo, Mkurugenzi Mkuu wa mgodi huo Bwana Josephat Muniko Mwita ameeleza kuwa uchimbaji wa madini katika mgodi huo ulianza tangu mwaka 1937 na umekuwa ukifanywa na wamiliki tofauti watano.
Bwana Mwita ameeleza kuwa aliununua mgodi huo baada ya kupata ruzuku kutoka serikalini mwaka 2007 na tangia hapo amekuwa akiendelea na shughuli za uchimbaji mpaka sasa
Bwana Mwita ameeleza kuwa kwa sasa mgodi huo umeajiri wafanyakazi 150 wenye ajira za kudumu na ajira za muda na ameshachangia pato la taifa zaidi ya shilingi milioni 500 kama kodi na ushuru wa huduma na kupanda miti 10,000 katika eneo la mgodi huo.
Aidha, Bwana Mwita ambaye pia ni mmiliki wa mgodi huo ameeleza kuwa mgodi huo umekuwa ukipokea wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo ya uchimbaji madini kutoka vyuo mbalimbali hapa nchini.
Bwana Mwita ameeleza kuwa pamoja na mafanikio mbalimbali waliyoyapata mgodi huo unakabiliwa na changamoto ya mtaji wa kupanua zaidi shughuli zao, wananchi kutegesha karibu na eneo la mgodi ili walipwe fidia na gharama kubwa za kukodi vifaa vya utafiti.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara na maafisa wengine kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa