Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee kesho tarehe 29 Desemba, 2022 anatarajia kufanya ziara ya kukagua upanuzi na ukarabati wa mradi wa maji wa Mugango- Kiabakari unaotekelezwa kwa thamani ya shilingi bilioni 70.5 unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji ya Mugango- Kiabakari.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara imeeleza kuwa Mheshimiwa Mzee atawasili katika ofisi za mradi huo eneo la Mugango na kupokea taarifa ya mradi huo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji ya Mgango- Kiabakari.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa baada ya hapo, Mheshimiwa Mzee atakagua chanzo cha maji cha mradi huo, ujenzi wa matenki mbalimbali ya kuhifadhi maji na ujenzi wa ofisi mpya za Mamlaka ya Maji Mugango- Kiabakari.
Upanuzi na ukarabati wa mradi wa maji wa Mugango- Kiabakari ulianza kutekelezwa mwaka 2020 na kuwekewa jiwe la msingi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 6 Februari, 2022 na ulitarajiwa kukamilika Desemba, 2022.
Awali, mradi huu ulijengwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza miaka ya 1970 lakini kutokana na ongezeko la mahitaji ya maji na uchakavu wa miundombinu mradi huu unakarabatiwa na kupanuliwa ili kuweza kuhudumia wananchi 165,000 kutoka vijiji 39 vya Wilaya ya Musoma na Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa