Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo ametangaza rasmi ratiba ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itakayofanyika katika Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 4 -7 Februari, 2022.
Mheshimiwa Hapi ametoa ratiba ya ziara ya Mheshimiwa Rais leo tarehe 1 Februari, 2022 katika mkutano na Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mara uliofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Mheshimiwa Rais atapokelewa Bunda Mjini tarehe 4 Februari 2022 mchana baada ya hapo anatarajiwa kusalimiana na wananchi wa eneo la Kiabakari lililopo katika Wilaya ya Butiama” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa tarehe 5 Februari, 2022, Mheshimiwa Rais anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 45 ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo kitaifa yatafanyika katika Uwanja wa Karume, Manispaa ya Musoma.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, tarehe 6 Februari, 2022 Mheshimiwa Rais anatarajiwa kuweka jiwe la msingi katika Mradi wa Maji wa Mgango- Kiabakari pamoja na kuwasalimia wananchi wa eneo la Mgango lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Aidha siku hiyo Mheshimiwa Rais anatarajiwa kuweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kwangwa) iliyopo katika Manispaa ya Musoma na kuzungumza na wananchi wa eneo la Kwangwa.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa tarehe 7 Februari, 2022 Mheshimiwa Rais anatarajiwa kutembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa katika eneo la Mwitongo, Wilayani Butiama na baadaye kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa chujio la maji, katika Mradi wa Maji wa Bunda, liliopo katika eneo la Nyabehu, Wilaya ya Bunda.
Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais anatarajiwa kuhitimisha ziara yake kwa kuzungumza na wananchi wa Mji wa Bunda katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika viwanja vya sabasaba.
Mheshimiwa Hapi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi katika maeneo ambayo Mheshimiwa Rais atakapopita, maeneo atakayosalimiana na wananchi na atakapofanya mikutano ya hadhara na kumshangilia.
Aidha Mheshimiwa Hapi amewaalika Watanzania wote kujitokeza kwa wingi katika Maadhimisho ya Miaka 45 ya CCM ambapo Mkoa wa Mara umepewa heshima wa kuwa mwenyeji wa tukio hilo la kihistoria kwa Chama cha Mapinduzi.
Hii ni ziara ya kwanza ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tangu alivyoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Machi 2020.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa