Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amepokea taarifa za maandalizi ya mbio za mwenge wa uhuru kutoka Wilaya na Halmashauri za Mkoa wa Mara na kuzitaka Wilaya kuongeza nguvu katika maandalizi yam bio za mwenge za mwaka 2025.
“Angalieni mapungufu ya mwaka jana muone ni maeneo gani yanahitaji kurekebishwa kwa haraka kwa kuzingatia vigezo vya mbio za mwenge wa uhuru mwaka huu” amesema Mhe. Mtambi
Mhe. Mtambi amewatahadhalisha kuwa bila maandalizi ya kutosha, Mkoa utapata aibu na kuwahakikishia kuwa uongozi wa Mkoa hautakubali kuaibika na kuwataka Wakuu wa Wilaya kuzisimamia Halmashauri kikamilifu.
Mhe. Mtambi amewataka Wakuu wa Wilaya na Kamati za Usalama za Wilaya kutembelea miradi iliyoainishwa na Halmashauri mapema ili kutoa nafasi za maandalizi kukamilika katika miradi itakayokubaliwa.
Mhe. Mtambi ameipongeza Wilaya ya Butiama kwa kuanza kufanya vikao vya maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru na kukagua miradi itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 na kuipongeza taarifa ya maandalizi na mipango ya Wilaya ya Serengeti iliyowasilishwa katika kikao hicho.
Mhe. Mtambi ameitaka Wilaya ya Musoma kuboresha shughuli za hamasa ya mwenge wa uhuru kwa mwaka 2025 na kumtaka Katibu Tawala wa Mkoa kuitumia Brass Band ya SENAPA katika mapokezi na makabidhiano ya Mwenge na kumshirikisha Mhe. Julius Masubo Kambarage katika maandalizi ya mbio za mwege wa uhuru katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mbio za Mwenge Mkoa wa Mara Bwana Fidel Baragaye ameeleza kuwa kwa mwaka huu mbio za mwenge zitaingia katika Mkoa wa Mara tarehe 15 Agosti, 2025 kutokea Mkoa wa Simiyu na kukimbizwa katika Halmashauri zote tisa na kukabidhiwa Mkoa wa Mwanza tarehe 24 Agosti, 2025 katika Wilaya ya Ukerewe.
Bwana Baragaye amesema kwa mwaka 2025, Mwenge wa Uhuru hautapitia miradi iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru, ukaguzi wa miradi utakwenda sambamba na ukaguzi wa miundombinu ya zamani, mwenge utakagua kisayansi kwa kutumia vifaa vya kisasa na mwenge utaenda katika maeneo ambayo hayajapitiwa na Mwenge wa Uhuru.
Bwana Baragaye amesema ujumbe wa mbio za mwenge kwa mwaka 2025 inahusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ukiwa na kauli mbiu “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 Amani na Utulivu”.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizinduliwa tarehe 02 Aprili, 2025 katika Mkoa wa Pwani na kilele cha Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Wiki ya Vijana Kitaifa tarehe 14 Oktoba, 2025 katika Mkoa wa Mbeya.
Katika kikao hicho, Halmashauri zote za Mkoa wa Mara zimewasilisha taarifa kuhusu maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 ikiwa ni pamoja na mikakati ya kuboresha katika mwaka 2025
Kikao cha tathmini ya mbio za mwenge mwaka 2024 na maandalizi ya mbio za mwenge 2025 kimehudhuriwa na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Waratibu wa Mbio za Mwenge wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa