Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Mara kubuni vyanzo vipya na endelevu vya mapato ili kuweza kuboresha makusanyo ya Halmashauri hizo na huduma kwa wananchi.
Akizungumza leo katika kikao cha tathmini ya utendaji kazi Mkoa wa Mara kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji, Mhe. Mtanda amezipongeza Halmashauri zilizofanya vizuri katika makusanyo ya robo ya kwanza na robo ya pili ya mwaka wa Fedha 2023/2024.
“Bila kuwa na mapato ya kutosha na endelevu, Halmashauri hazitaweza kutekeleza majukumu yake na hivyo kushindwa kujiendesha katika masuala ya msingi ya kuwahudumia wananchi kutokana na ukosefu wa fedha” amesema Mhe. Mtanda.
Aidha, amezitaka Halmashauri kuacha kutegemea vyanzo vya mapato ambavyo havina tija tena kama vile uvuvi na kilimo ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa havifanyi vizuri lakini ndio vyanzo vikuu vya mapato kwa baadhi ya Halmashauri.
Mhe. Mtanda amezishauri Halmashauri kuwekeza katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ili kuwezesha wananchi kuzalisha samaki kwa wingi na hivyo kuongeza samaki katika Ziwa Victoria na hatimaye kuongeza mapato ya Halmashauri.
Amewataka Wakuu wa Wilaya na viongozi wa Halmashauri kutoa msukumo zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri na kuwataka Maafisa Mipango wa Halmashauri kufanya ushirikishaji wa kutosha katika kubuni mipango ya Halmashauri zao.
Mhe. Mtanda amezitaka Halmashauri kuwafuatilia kwa ukaribu wakusanya mapato na kuhakikisha kuwa wanakusanya kupitia mfumo na wanaweka fedha benki kwa wakati kwa mujibu wa makubaliano ya mikataba yao.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amezitaka Halmashauri zote kuhakikisha kuwa watoto wote waliopaswa kuanza darasa la awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza wanaenda shule na kuanza masomo kabla ya tarehe 31 Marchi, 2024.
Amewataka Wakuu wa Divisheni za Elimu kwa kushirikiana na viongozi na watendaji mbalimbali kufanya msako wa nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha watoto wote wanaenda shule kuanza masomo yao kwa mwaka 2024.
Awali akitoa taarifa ya uandikishaji, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bwana Bulenga Makwasa amesema kwa sasa masomo yameshaanza japokuwa muda wa kupokea watoto bado upo hadi tarehe 31 Machi, 2024.
Bwana Makwasa amewaomba viongozi kushirikiana ili kuwawezesha watoto wengi zaidi kuanza masomo na kunufaika na elimu bure inayotolewa kuanzia madarasa ya awali hadi Kidato cha Sita hapa nchini.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa