Mkutano Mkuu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Mara umefanyika leo katika ukumbi wa Uwekezaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na kufunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee.
Akifungua mkutano huo, Mheshimiwa Mzee ameyapongeza mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoa wa Mara kwa kutoa huduma mbalimbali kwa jamii ambazo zinawasaidia wananchi na kuwakwamua kwenye baadhi ya changamoto zinazowakabili.
“Napenda kuwapongeza kwa namna mnavyoshirikiana na Mkoa katika kutoa huduma mbalimbali kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa elimu, miundombinu, msaada wa kisheria, utunzaji wa mazingira na kadhalika, hii inachochea maendeleo ya Mkoa wetu” alisema Mheshimiwa Mzee.
Hata hivyo Mheshimiwa Mzee ameyataka mashirika hayo katika utendaji wao kuacha alama katika maeneo wanayofanyia kazi ili hata miradi yao inapokuwa imeisha muda wake, jamii iwe na kumbukumbu nzuri ya miradi hiyo.
Aidha, Mheshimiwa Mzee ameyataka mashirika hayo kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa usajili wao na kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za utekelezaji wa majukumu kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kupitia Msajili wa Mashirika yasiyo ya kiserikali.
Kwa upande wake, Msajili Msaidizi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Mara Bibi Neema Ibamba ameeleza kuwa lengo la mkutano huo ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu uratibu na usimamizi wa Mashirika Yasiyo ya Kisherikali katika maendeleo ya Mkoa wa Mara.
Bibi Ibamba ameeleza kuwa Mkoa wa Mara unajumla ya mashirika 286 yasiyo ya kiserikali lakini katika hayo mashirika 156 yapo hai lakini mashirika 130 hayapo hai na yanatarajiwa kufutwa kutokana na kutotmiza masharti na vigezo hususan kutokulipa ada.
“Ninaomba kuwasisitiza tutimize wajibu wetu ikiwa ni pamoja na kulipa ada, kutoa taarifa za utekelezaji wa majukumu na bajeti kwa mujibu wa sheria na taratibu za usajili” alisema Bibi Ibamba.
Bibi Ibamba ameyataka mashirika yaliyo katika orodha ya kufutwa, kufuata sheria na taratibu kwa kushirikiana na wasajili wasaidizi wa Mkoa na Halmashauri ili mashirika hayo yaweze kurudishiwa usajili na kuendelea na majukumu yao.
Aidha, Bibi Ibamba amewahamasisha wadau wote kujisajili kupitia http://register.jamii.go.tz ili kuweza kushiriki katika mkutano wa kitaifa wa mashirika yasiyo ya kiserikali utakaofanyika Dodoma tarehe 03-04 Oktoba, 2022.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu na viongozi wa Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Mara ambao walitumia fursa hiyo kujitambulisha kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Mkoa wa Mara.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya Mkoa wa Mara, Maafisa Maendeleo ya Jamii ambao ni Wasajili Wasaidizi wa Mashirika hayo ngazi za Halmashauri na Mkoa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa