Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo amezindua mradi wa utafiti wa “Kuhamasisha Uanzishaji wa Ajira na Miradi ya Kiuchumi kwa Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu” unaofadhiliwa na Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Maendeleo (IRDC) cha Canada.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Mzee amewataka watafiti hao kuhakikisha wanaufanya utafiti huo na kutoa matokeo ya utafiti huo kwa haraka ili Serikali ikiyafanyia kazi mapungufu yaliyopo iweze kuwasaidia wananchi.
“Matokeo ya utafiti huu tunatarajia yapunguze athari za mapungufu yanayoendelea kwa sasa katika utoaji wa mikopo ya makundi maalum kwa Halmashauri zetu, sasa yakichelewa sana hayatakuwa na manufaa tunayoyatarajia” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, ametoa changamoto kwa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kuhakikisha wasomi watakaopita katika Chuo hicho wanajiajiri na wanaajiri wengine ili kupunguza uhaba wa ajira hapa nchini.
Kwa upande wake Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) Prof. Lesakit Mellau ameeleza kuwa mradi huo utafanyika katika kipindi cha miaka mitatu na gharama ya mradi mzima ni shilingi milioni 910.
Prof.Mellau ameeleza kuwa mradi huo unaunganisha mafunzo kwa wahadhiri watatu mmoja katika Shahada ya Uzamivu na wawili katika Shahada ya Uzamili pamoja na utafiti utakaofanyika katika Mikoa ya Mara na Arusha.
Ameeleza kuwa kwa Mkoa wa Mara utafiti utafanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Halmashauri ya Mji wa Bunda, Manispaa ya Musoma, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, na Halmashauri tatu za Mkoa wa Arusha ambazo ni Halmashauri ya Jiji la Arusha, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na Halmashauri ya Wilaya ya Longido.
Prof. Mellau ameeleza kuwa dhima ya Chuo hicho ni Pata Elimu, Jiajiri, Tengeneza Ajira ambayo inalengo la kuhamasisha wanachuo wa Chuo hicho kusoma kwa bidi ili kuja kujiajiri na kutengeneza ajira za kuajiri watu wengine.
Uzinduzi wa utafiti huo umehudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, wataalamu wa Chuo hicho, Wakurugenzi wa Halmashauri zitakazopitiwa na utafiti, mashirika yasiyo ya kiserikali na watafiti watakaohusika katika Mradi huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa