Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amewataka watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kujali maendeleo ya wananchi wa Bunda katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mheshimiwa Malima ametoa kauli hiyo leo tarehe 5 Juni 2020 wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa ajili ya kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
“Hoja hizi nyingi za CAG ni matokeo ya utendaji mbaya wa kutokuzingatia sheria na kanuni mbalimbali na zinapokuwa zinajirudia mara nyingi ineleta shida kuwaelewa watendaji” alisema Mheshimiwa Malima.
Aidha amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kuhakikisha mapendekezo ya CAG kuhusiana na kitengo cha Ukaguzi wa Ndani yanafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuongeza watumishi, bajeti na idara kupatiwa gari kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.
Mheshimiwa Malima amemtaka Mkurugenzi na watendaji wote kuzingatia kanuni za fedha na sheria nyingine katika utekelezaji wa majukumu yao.
Halmashauri ya Wilaya ya Bunda katika taarifa ya CAG ya mwaka 2018/2019 imepata hati safi. Hata hivyo ina hoja 109 ambapo kati yake hoja 73 za miaka ya nyuma kuanzia mwaka wa fedha 2012/2013 na hoja mpya 36 za mwaka wa fedha 2018/2019.
Kati ya hoja hizi, hoja nyingi zimejibiwa na nyingine utekelezaji wake uko katika hatua mbalimbali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa