Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee leo tarehe 9 Agosti, 2022 ametembelea Hospitali ya Wilaya ya Butiama inayoendelea kujengwa na kuwataka wasimamizi wa miradi ya maeendeleo kusimamia kwa umakini utekelezaji wa miradi ya Serikali.
Mheshimiwa Mzee ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea majengo mbalimbali yanayoendelea kujengwa katika katika Hospitali hiyo na kubaini changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa mradi huo.
“Haiwezekani Serikali inatoa fedha za ujenzi wa miradi halafu tunasimamia miradi inayotekelezwa hovyo hiyo bila kuangalia ubora na utekelezaji wa mradi kwa wakati” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee ameagiza kuondolewa kwa milango yote iliyofungwa katika jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na kuimarisha nondo za madirisha zilizowekwa pamoja na kurekebisha upigaji wa plasta, rangi na uwekaji wa vigae katika jengo hilo.
Aidha, Mheshimiwa Mzee amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Butiama kuusimamia mradi huo kwa karibu na kuwaondoa mafundi ambao hawatekelezi mradi huo kwa wakati kwa kufuata sheria na taratibu.
Awali akitoa taarifa za mradi huo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Bwana Deusdedit Kalaso ameeleza kuwa Halmashauri hiyo imepokea jumla ya shilingi bilioni 1.3 kwa awamu tatu tofauti kuanzia Mei, 2021 kwa ajili ya kujenga majengo manne.
Kwa mujibu wa Dkt. Kalaso majengo yanayojengwa kwa sasa ni pamoja na jengo la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, wodi ya mama na mtoto na jengo la wagonjwa wa dharura.
Dkt. Kalaso ameeleza kuwa ujenzi wa hospitali hiyo unaendelea vizuri na kwa sasa majengo yote yapo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu, Viongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa