Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo amewataka waanchi wa Kata ya Nyanungu, katika Wilaya ya Tarime kulitumia vizuri eneo la mlima linalopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) kwa maendeleo ya uhifadhi na utalii na kuacha mara moja shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Mzee amesema hayo kwa nyakati tofauti tofauti wakati alipoambatana na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kamati ya Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Tarime kukagua eneo hilo kwa lengo la kusuluhisha mgogoro baina ya wananchi na SENAPA.
“Mkilitumia eneo hili kwa kuwaita wawekezaji wa kujenga hoteli za kitalii, mtakuwa matajiri na mtaachana na migogoro baina yenu na watumishi wa SENAPA waliokasimiwa na Taifa kuilinda Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ” amesema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee amewataka wananchi hao kuangalia mfano wa nchi ya Kenya ambayo imetumia eneo lilalopakana na mlima huo kwa upande wa Tanzania kuweka vivutio vya watalii na kulitumia vizuri eneo lao.
“Tuangalie majirani zetu tunaopakana nao hapa, wao wanalitumia eneo lao kwa ajili ya shughuli ya utalii, na katika eneo lao Serengeti haionekani vizuri kama ukiwa hapa tulipo, lakini sisi hapa tunalima humu kwenye mawe na tunachokipata hakina tija hata kwa mkulima mwenyewe” amesema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee amewataka wananchi kuheshimu mpaka kati ya vijiji hivyo na SENAPA ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara katika eneo hilo na badala yake wajikite kwenye kujenga mahusiano na ujirani mwema na SENAPA.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Mzee amekemea kitendo cha wananchi wa eneo hilo kumuua askari wa SENAPA kwa mshale wa sumu akiwa katika eneo la Hifadhi akitekeleza majukumu yake na kuwakemea wanasiasa wanaowahamasisha wananchi kutembea umbali mrefu ndani ya hifadhi ili kunywesha mifugo katika Mto Mara uliopo ndani ya hifadhi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara Mheshimiwa Patrick Chandi Marwa amewasihi wananchi kuitumia fursa hiyo vizuri na kuliomba Shirika la Hifadhi za Tanzania (TANAPA) kuwapeleka wawekezaji wakubwa katika eneo hilo.
“Mwekezaji huyo aingie mkataba na vijiji hivi ili mapato yanayotokana na uwekezaji huo yabadilishe maisha ya wananchi wa eneo hili na kuachana na migogoro isiyokuwa na tija” amesema Mheshimiwa Chandi.
Mheshimiwa Chandi amewapa mfano wa Kijiji cha Natta kilichopo katika Wilaya ya Serengeti ambacho ambacho kina milima miwili midogo kuliko Nyanungu na wananchi wameruhusu uwekezaji na sasa Kijiji kinapata shilingi bilioni tatu kila mwaka kutoka kwa uwekezaji huo.
Eneo la vijiji vitano katika Kata ya Nyanungu vipo katika mlima wenye madhari ya kipekee unaowezesha watu kuitazama sehemu kubwa ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na na hivyo kufaa kwa ajili ya uwekezaji wa hoteli za kitalii.
Taarifa iliyotolewa na wataalamu wa TANAPA inaonyesha kuwa kufuatia maagizo ya Baraza la Mawaziri kuhusu matumizi ya eneo la kinga (buffer zone) katika vijiji vitano vya Kata ya Nyanungu, vijiji vya Kegonga na Nyandage vimegomea kuwekewa vigingi vya mpaka wakati vijiji vya Gibaso, Masanga na Karakatonga wamekubali kuwekewa alama za mipaka na kuruhusu kupimiwa eneo lao.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa