Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo tarehe 11 Septemba, 2022 amekutana na wafanya biashara wadogo wa madini katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na kuwataka wafanyabiashara hao kufanya biashara kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali.
Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Mzee amesema ameshatembelea migodi yote ya madini katika Mkoa wa Mara na kugundua kuwa baadhi ya wafanyabiashara wa madini wanafanya biashara hiyo kiujanja ujanja ili kukwepa kulipa maduhuli stahiki ya Serikali.
“Mkilipa vizuri kodi, mrahaba na ushuru wa huduma itakuwa rahisi kupata huduma za kijamii katika maeneo yenu mnapofanyia biashara ikiwa ni pamoja na barabara, hospitali, maji na shule, na mimi nitahakikisha mnapata huduma bora” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee pia amewataka wafanyabiashara wadogo wote wa madini kukata leseni halali za biashara ili kuwawezesha kuwa huru katika kufanya biashara zao.
Kwa upande wake, Bwana Jakson Ngassa ameiomba Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuanza haraka mchakato wa kununua madini ya dhahabu ili wafanyabiashara wa madini wasiathirike na kushuka kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia.
“Hii itatusaidia sisi ambao hatuna mtaji mkubwa kuweza kuhimili ushindani wa kibiashara katika soko la dunia” amesema Bwana Ngassa.
Bwana Ngasa ameeleza kuwa kutoka kwenye uchimbaji soko liko vizuri, lakini katika soko la dunia bei ya dhahabu inacheza sana na wafanyabiashara wengi wanapata hasara kubwa katika hiyo bei.
Aidha, kwa upande wao wafanyabiashara kutoka Mgodi wa Irasanilo uliopo katika eneo la Buhemba, Wilaya ya Butiama wamelalamikia kukosekana kwa mahitaji muhimu katika eneo hilo hususan hospitali.
“Wachimbaji wengi wanapoteza maisha kutokana na umbali kutoka eneo la mgodi hadi ilipo hospitali, na katika uchimbaji ajali zinatokea mara kwa mara” walisema wafanyabiashara hao.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa