Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee leo tarehe 16 Agosti, 2022 amewataka wadau wote wa Sensa ya Watu na Makazi katika Mkoa wa Mara kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 itakayofanyika tarehe 23 Agosti, 2022.
Mheshimiwa Mzee ameitoa kauli hiyo leo katika kikao cha uhamasishaji wa sensa kwa viongozi wa dini, vyama vya siasa, Shirikisho la Wafanyabiashara, wazee wa mila na Waandishi wa Habari kilichofanyika katika ukumbi wa uwekezaji uliopo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Ninatambua umuhimu wa kila kundi lililopo hapa, na kwa sababu suala la Sensa ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu, ninaomba kila mmoja wetu kwenye eneo lake atumie muda uliobakia kuwahamasisha wananchi hasa wale ambao hawajaelewa kuhusu zoezi la Sensa” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa wananchi wanapaswa kupewa elimu juu ya sensa ili waweze kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Amewataka Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mara kutumia vyombo vyao vya ndani ya Mkoa, kitaifa na kuwashirikisha waandishi wa nchi jirani kutoa elimu ya sensa kwa wananchi wa Mkoa wa Mara ili waweze kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.
Amewahamasisha wadau kuwahamasisha wananchi wote kuwatoa watu wenye ulemavu waliopo katika maeneo yao ili waweze kuhesabiwa kiurahisi. “Ukiwa na ndugu mlemavu, usimfiche, kujulikana kwake ndio itakuwa rahisi kwake kusaidiwa katika ulemavu wake” alisema Mheshimiwa Mzee.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mheshimiwa Samwel Kiboye ameeleza kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kimekuwa kikihamasisha Sensa ya Watu, 2022 na Makazi katika maeneo mbalimbali.
Amewataka wadau walioshiriki katika kikao hicho kuacha masuala mengine yote na kuitangaza Sensa kwa muda huu uliobakia ili iweze kufanyika kwa ufanisi zaidi.
Aidha, ameahidi kutoa ushirikiano kuhakikisha zoezi la Sensa linafanikiwa na Mkoa wa Mara unafanya vizuri katika zoezi la Sensa.
Kikao cha wadau wa Sensa kilifanyika ikiwa ni sehemu ya uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 na kuhudhuriwa na wawakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa