Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo amefungua kikao cha Wadau wa Mfuko wa Maendelea ya Jamii (TASAF) katika Mkoa wa Mara na kuwataka viongozi na watendaji wa Mkoa wa Mara wajitathmini na kujirekebisha kabla hajachukua hatua.
Mheshimiwa Mzee ametoa kauli hiyo baada ya kupokea taarifa ya zoezi la kuwaingiza wanufaika wa TASAF katika mfumo ili waweze kupata malipo yao kupitia benki na simu za mkoanoni katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini unaofadhiliwa na TASAF halijaenda vizuri kutokana na changamoto mbalimbali.
“Haiwezekani wanufaika wa mpango huu washindwe kupata fedha kupitia katika simu au benki na Waratibu wa TASAF ngazi ya Halmashauri na Mkoa mpo na mnaileta hapa hoja kama ni changamoto wakati hamjachukua hatua yoyote kuitatua changamoto hiyo” alisema Mkuu wa Mkoa.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amesema anatamani aone kila mmoja anawajibika katika eneo lake na kuachana na visingizio ambavyo havitatui changamoto za wananchi wa Mkoa wa Mara na kuinua maendeleo ya Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mzee amewaagiza Waratibu wa TASAF katika Halmashauri kuhakikisha kuwa wanufaika wa mpango huo wanasaidiwa kupata vitambulisho au namba za utambulisho kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Kwa upande wake, Meneja Mtaalamu wa Ufuatiliaji na Uwezeshaji kutoka TASAF Makao Makuu Bibi Salome Mwakigomba ameeleza kuwa TASAF ilianzisha utaratibu wa kuwalipa wanufaika kutumia taasisi za kifedha ili kuboresha ulipaji wa fedha kwa walengwa wa mpango huo.
Bibi Mwakigomba amewataka Waratibu wa TASAF kuhakikisha kuwa wanufaika wanaingizwa katika mfumo wa malipo ili waweze kupata malipo yao kwa wakati na kupunguza usumbufu wa wananchi kufuata malipo katika vituo vya kulipia.
Aidha, amewataka waratibu wa TASAF kufanyiakazi orodha ya wanufaika wanaotarajiwa kuondolewa katika mfumo baada ya taarifa kuonyesha kuwa wanauwezo wa kujitegemea na kuendesha maisha yao bila ya msaada wa Serikali.
Bibi Mwakigomba amewaomba Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa shughuli za TASAF kwa manufaa ya Halmashauri na wananchi wanaowatumikia katika maeneo yao.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Dominicus Lusasi ameeleza kuwa kikao cha leo kilikuwa na lengo la kuwaeleza wadau shughuli za TASAF zilizofanyika; mafanikio ya Mpango yaliyopatikana; changamoto zilizopatikana; na mikakati iliyopo kutatua changamoto hizo.
Aidha, Bwana Lusasi ameeleza kuwa wadau watapata muda wa kufanya majadiliano na hatimae kuwa na mikakati ya pamoja katika kupunguza ama kumaliza kabisa changamoto za utekelezaji wa mpango katika Mkoa wa Mara.
Bwana Lusasi ameeleza kuwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ni kaya 63,346 zenye idadi ya watu 316,730.
Bwana Lusasi ameeleza kuwa mpango huo una sehemu nne ambazo ni uhawalishaji wa fedha kwa kaya masikini unaofanyika kupitia kutoa ruzuku kwa kaya maskini na kutoa ajira za muda kwa watu wanaotoka kaya masikini; kuongeza kipato kwa kaya maskini kupitia uwekaji wa akiba na shughuli za kiuchumi; kujenga na kuboresha miundombinu ya sekta za Afya, Elimu na Maji; na kujenga uwezo katika ngazi zote za utekelezaji.
Kikao hicho kilihudhuliwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Waurugenzi wa Halmashauri, Waratibu wa TASAF wa Halmashauri na wadau mbalimbali kutoka taasisi za umma na binafsi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa