Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Suleiman Mungiya Mzee leo amewapongeza wananchi wa Mtaa wa Kogesenda, Kata ya Mkenda kwa kujenga maboma 8 ya vyumba vya madarasa, ofisi 4 za walimu na kuanza ujenzi wa matundu ya vyoo vya walimu na wanafunzi katika Shule mpya ya Sekondari Magena.
Akizungumza baada ya kukagua madarasa hayo na ofisi za walimu, Mheshimiwa Mzee amesema walichokifanya wananchi hao ni mfano wa kuigwa na wapenda maendeleo wote hapa nchini.
“Huu ni mfano wa kuigwa sio tu kwa wananchi wa Tarime na Mkoa wa Mara bali ni Watanzania wote, jambo mlilolifanya ni zuri sana na la kimaendeleo yenu na vizazi vijavyo” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee amechangia shilingi milioni 2 kuunga mkono juhudi za wananchi wa Mtaa wa Kogesenda ili waweze kukamilisha ujenzi wa vyoo katika Shule ya Sekondari Magena kuwataka watu wote alioambatana nao kuchangia walichonacho ili kukamilisha ujenzi wa vyoo hivyo.
Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Tarime Kanali Maichael Mtenjela kuitisha kikao na wananchi tarehe 6 Januari, 2023 kwa ajili ya kuweka sawa wananchi baada ya Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini kuwaambia wananchi hao wasiendelee kuchangia ujenzi wa shule hiyo yeye anatoa pesa.
“Kwa kuwa pesa inayotolewa na Mbunge haiwezi kukamilisha ujenzi wa vyoo hivi, zungumza na wananchi waendelee kuchangia na kuweka sawa mapungufu yote yaliyopo katika uchangiaji huo wa wananchi ili Shule iweze kuchukua wanafunzi Januari 2023” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee ameitaka Halmashauri ya Mji wa Tarime kuwasaidia wananchi hao kwa haraka kukamilisha ujenzi wa vyoo ili iweze kusajiliwa na kupokea wanafunzi Januari, 2023 kama ilivyopangwa awali.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kogesanda Bwana Paulo Waheke Keraryo ameeleza kuwa wananchi wake wamechangia ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa na kujenga maboma hayo ndani ya miezi 7 na maboma yakawa yamekamilika na kuanza ujenzi wa vyoo.
“Kwa sasa tumeanza ujenzi wa vyoo vya walimu na wanafunzi lakini juhudi zetu zimekwama baada ya Mbunge wa Tarime Mjini kuwaambia wananchi wasichangie tena yeye atatoa shilingi milioni nne, fedha ambayo haiwezi kukamilisha ujenzi wa matundu ya vyoo yanayohitajika” alisema Bwana Keraryo.
Bwana Keraryo amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuchangia shilingi milioni 2 jambo ambalo limewatia moyo kuendelea kuchangia kukamilisha ujenzi wa vyoo hivyo.
Aidha, Bwana Keraryo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha shilingi milioni 100 ambazo zimewezesha ukamilishaji wa vyumba vya madarasa na ofisi hizo.
Bwana Keraryo ameeleza kuwa Shule ya Sekondari ya Magena itakapoanza itawapunguzia umbali wa kutembea wanafunzi wa kidato cha kwanza watakaoanza kusoma katika shule hiyo na kuongeza ari ya wanafunzi kuipenda shule na kujifunza.
Tayari mashimo ya vyoo katika shule hiyo yameshajengwa, kwa sasa maandalizi ya ujenzi wa maboma ya vyoo hivyo yanaendelea na vinatarajiwa kukamilika kabla ya tarehe 9 Januari, 2023.
Katika kutembelea Sekondari ya Magena, RC aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Elimu, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Miundombinu, Kaimu Katibu Tawala Msadizi Mipango na Uratibu, maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mkurugenzi na Menejimenti ya Halmashauri ya Mji wa Tarime na viongozi wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa