Mkuu wa Mkoa wa Mara leo tarehe 11 Septemba, 2022 amekutana na Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodini na Nishati (NUMET) ambao wamemtembelea ofisini kwake kwa ajili ya kujitambulisha na kuwapongeza kwa namna wanavyopigania maslahi ya wafayakazi wa sekta ya madini na nishati hapa nchini.
“Kazi mnayoifanya ni kubwa sana na niwaombe muendelee kuifanya ili kuwatetea wafanyakazi katika migodi mbalimbali iliyopo hapa nchini” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee amewataka viongozi hao kutoa ushirikiano kwa Serikali wakati wa kutekeleza majukumu yao ili kuiwezesha serikali kuchukua hatua stakihi kama kuna tatizo.
Amewahakikishia viongozi hao ushirikiano kutoka kwa viongozi wote wa Mkoa wa Mara katika kutekeleza majukumu yao ya kusimamia haki za wafanyakazi katika sehemu zao za kazi.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Katibu Mkuu wa NUMET Bwana Nicomedes Kajungu ameeleza kuwa wamefurahi kupata fursa ya kukutana na Mkuu wa Mkoa na kuweza kuwasilisha changamoto mbalimbali wanazokutana nazo kutoka kwa wafanyakazi.
Bwana Kajungu ameeleza kuwa NUMET ilianzishwa mwaka 2013 na mpaka sasa ina wanachama 4,339 kutoka katika matawi 37 nchi nzima yakiwemo matawi 10 kutoka Mkoa wa Mara.
NUMET ameeleza kuwa kwa sasa NUMET imeshawafikia wafanyakazi katika migodi yote mikubwa hapa nchini na kufanikiwa kunusuru ajira za wafanyakazi zaidi ya 1,000 kwa kushirikiana na Mamlaka ya Ushuluhishi wa Migogoro mahali pakazi (CMA).
Bwana Kajungu ameeleza kuwa NUMET imeendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali walizozibaini ikiwa ni pamoja na mikataba ya muda mfupi isiyokidhi matakwa ya sheria; baadhi ya waajiri kutolipa masaa ya ziada; na baadhi ya waajiri kutowasilisha michango ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Amesema changamoto nyingine kuwa ni waajiri kutokulipa mshahara wakati watumishi wakiwa likizo, malipo ya mshahara kinyume na kima cha chini cha mshahara; ukosefu wa vifaa vya usalama; wafanyakazi kutopewa huduma za msingi; ukiukwaji wa haki za vyama; na ucheleweshaji wa kanuni za usimamizi wa sheria.
Aidha, Bwana Kajungu amezitaja changamoto nyingine kuwa ni manyanyaso ya vipigo na udhalilishaji; malipo ya kima cha chini yasiyokidhi mahitaji ya msingi kwa wafanyakazi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa