Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amekutana na kuzungumza na Kamati ya Amani na Maridhiano ya Mkoa wa Mara katika Ukumbi wa Uwekezaji na kuwaomba viongozi wa dini kukemea maovu katika jamii.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa amewashukuru viongozi hao kwa kukutana nae na kuwaomba kuisaidia Serikali katika kukemea maovu mbalimbali katika jamii ikiwemo kukemea wananchi wanapochukua sheria mkononi kunapokuwa na jambo ambalo linaweza kutatuliwa kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.
“Ninawaomba katika mahubiri yenu kukemea vitendo viovu katika jamii ikiwa ni pamoja na mauaji ya mara kwa mara yasiyo na sababu za msingi ambayo yapo katika jamii na kupunguza ukatili kwa kupigana kwa kutumia silaha katika migogoro ya kifamilia na kijamii” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewaomba viongozi wa dini kukemea na kuliweka katika maombi suala la ulawiti na ubakaji wa watoto wadogo mashuleni na katika jamii na kukemea migogoro ya ardhi inayosababishwa na ongezeko la idadi ya watu, mifugo na shughuli za kibinadamu katika ardhi iliyopo.
Aidha, Mhe. Mtambi amewataka viongozi hao kukemea kilimo cha madawa ya kulevya aina ya bangi na mirungi kinachofanywa na baadhi ya wananchi katika Mkoa wa Mara kwani madhara yake katika jamii ni makubwa sana.
Mhe. Mtambi amesema kuanzia sasa, Kamati hiyo itakuwa na kikao na Mkuu wa Mkoa kila mwezi kujadili masuala mbalimbali na itaanzisha maombi ya pamoja ya kuliombea Taifa, viongozi na Mkoa wa Mara na wananchi wake.
Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Amani na Maridhiano Mkoa wa Mara Shehe Juma Masiloli akisoma taarifa ya kamati hiyo amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Shehe Masiloli pia alitumia fursa hiyo kuwasilisha maombi ya Kamati hiyo ya kupatiwa shilingi 1,000,000 kwa ajili ya pango la ofisi na mafuta lita 140 kwa ajili ya ziara watakayoifanya katika Wilaya tatu za Mkoa wa Mara.
Aidha, Shehe Masiloli pia ameeleza kuwa baadhi ya viongozi wa taasisi za Serikali hawatoi ushirikiano kwa Kamati ya Amani na Maridhiano jambo ambalo linawawia vigumu kutekeleza majukumu yao na kuomba Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuwawezesha wanapohudhuria vikao vya kamati hiyo kitaifa.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Askofu Jacob Lutubija na wajumbe wengine wa Kamati hiyo pamoja na baadhi ya maofisa wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa