Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo amekutana na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na kuwataka wafanyakazi kuongeza ushirikiano baina ya wafanyakazi na viongozi ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mzee amesema kuwa kwa kawaida wafanyakazi wanatumia muda mwingi ofisini, kwa hiyo ni muhimu ofisini kuwe ni mahali pazuri kwa ajili ya kuishi, kwenye ushirikiano wa kutosha ili watu wafanye kazi zao kwa furaha.
“Mimi nimekuja kwa ajili yenu, mimi ni mtumishi wenu, mkifanya vizuri katika majukumu yenu mimi nitapewa sifa, lakini mkiharibu na mimi mtaniharibia pia, kwa hiyo tujitahidi kufanya kazi vizuri na kwa ushirikiano ili tuweze kuyafikia malengo yetu” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee amewashukuru wafanyakazi wa Ofisi a Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa mapokezi mazuri waliyompa wakati alipowasili kwa ajili ya kuanza kazi katika Mkoani Mara tarehe 6 Agosti, 2022.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa anapenda kuona mabadiliko yenye a kimaendeleo katika utendaji kazi na kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Mara.
Amewapa changamoto wafanyakazi kutafuta mradi au shughuli ya kiuchumi ya kufanya kwa pamoja itakayowaongezea wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na familia zao kipato ili waweze kujikimu kimaisha.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa anatamani atakapoondoka Mkoa wa Mara awe ameacha alama, na hiyo hawezi kufanya peke yake anahitaji ushirikiano wa watumishi wote katika kufanikisha azma yake ya kuiletea Mara maendeleo.
Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa katika kufanya kazi atawashirikisha wafanyakazi wote na kuongeza kuwa “kuweni huru na mimi, mtu akifanyakazi yake vizuri hatuwezi kugombana na tukiwa kwenye misingi ya kazi hatuwezi kuwa maadui” alisema Mheshimiwa Mzee.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Dominicus Lusasi ameeleza kuwa kwa sasa Mkoa wa Mara una wafanyakazi 178 ambao kati yao wafanyakazi 88 wapo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na wengine wapo katika ofisi za Wakuu wa Wilaya na ofisi za Maafisa Tarafa.
Bwana Lusasi ameeleza kuwa kwa sasa ofisi ya Mkuu wa Mkoa ina jumla ya Idara saba na vitengo sita kwa mujibu wa muundo mpya wa utumishi ulioanza kutumika katika Sekretarieti za Mikoa hapa nchini kuanzia tarehe 1 Julai, 2022.
Bwana Lusasi amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutenga muda wa kuzungumza na watumishi na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo aliyoyatoa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa