Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Sulaiman Mungiya Mzee leo amekutana na viongozi wa vyama vya Shirikisho la Watu wenye Ulemavu (SHIVIWATA) Mkoa wa Mara na kuvitaka vyama hivyo kuanzisha miradi ya uzalishaji mali ikiwa ni sehemu ya kuwakimu watu wenye ulemavu kiuchumi.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa Serikali kwa kutambua hali ya watu wenye ulemavu, imetenga fedha kupitia makusanyo ya ndani ya Halmashauri ili kuweza kutoa mikopo kwa ajili ya wananwake, vijana na watu wenye ulemavu.
“Hamuwezi kuwa na vyama vya watu wenye ulemavu ambavyo haviwasaidii wanachama wake, vinapaswa vyama hivi viwe na vyanzo vya mapato ili kuweza kuwapa wanachama wake manufaa yanayokusudiwa” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa bila vyama hivi kujihusisha na shughuli za uzalishaji mali, havitaweza kujiendesha na kuwasaidia wanachama wake inavyotakiwa na havitaweza kuwawezesha watu wenye ulemavu kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali.
“Bila kuwa na shughuli za uzalishaji mali itakuwa vigumu kwa mlemavu mmoja mmoja au hata kwa ujumla wenu kunufaika na fursa hiyo, hivyo ninashauri kwa kuwa tayari mpo katika vyama vya watu wenye ulemavu, vyama hivi vitumike kuwasaidia” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, amewataka watu wenye ulemavu kupambana ili kupata maisha bora na kuahidi kuwasaidia kama wataanzisha mradi wowote ambao utakuwa na tija.
Mheshimiwa Mzee pia amewaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwasaidia watu wenye ulemavu kuunda vikundi na kuanzisha miradi kulingana na hali halisi waliyonayo katika maeneo yao na kusaidiwa kupata mikopo ya Halmashauri ili waweze kuanzisha biashara.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa ametoa siku saba kwa Halmashauri za Wilaya za Butiama, Rorya, Musoma na Manispaa ya Musoma ambazo hazijazindua Kamati za Watu Wenye Ulemavu katika Halmashauri kuzindua Kamati hizo na kutoa taarifa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mzee ametoa maagizo hayo kufuatia taarifa ya SHIVIWATA kuonyesha kuwa Halmashauri hizo hazijazindua rasmi Kamati za Watu wenye Ulemavu ambazo zipo kwa mujibu wa Sheria.
Wakizungumza katika kikao hicho, viongozi wa SHIVIWATA wamemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa kukutana nao na kuuomba Mkoa kuwasaidia katika kufanikisha shughuli mbalimbali wanazozifanya kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Dkt. Zabron Masatu, maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii na maafisa wengine wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa