Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ametoa siku tatu kwa menejimenti ya Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) Musoma kutoa maelezo kwa nini haikutelekeza maagizo ya Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Butiama kuhusiana na taarifa za ujenzi wa Chuo cha VETA Butiama.
Mheshimiwa Hapi ametoa maagizo hayo leo tarehe 19 Julai 2021 baada ya kukagua na kutoridhishwa na utekelezaji wa mradi huo pamoja na taarifa ya mradi aliyosomewa katika eneo la mradi huo.
“Ninatoa siku tatu hadi tarehe 23 Julai, 2021 ninataka maelezo kwa nini taarifa mliyoelekezwa na kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Butiama hamkutekeleza” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha ametoa siku moja kwa Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha VETA Butiama kupitia Mkuu wa Chuo cha VETA Musoma kuwasilisha maelezo ofisini kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kesho tarehe 20 Julai 2021 kwa nini alikaidi maagizo ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama aliyompa kuhusiana na uandaaji wa taarifa za ujenzi wa chuo hicho kwa ajili ya ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Ninataka maelezo yake yapitia kwako ili tujue na hatua ulizopanga kuzichukua kwa mtendaji wako kukiuka maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama na yafike maelezo hayo kesho saa nne asubuhi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa lengo la ziara yake ilikuwa ni kufuatilia fedha za serikali zilivyotumika katika ujenzi wa Chuo hicho lakini taarifa anayosomewa haionyeshi fedha iliyotumika kwenye kila jengo la mradi huo kwa madai kuwa menejimenti ya VETA haijapiga hesabu za mradi huo hata baada ya kupatiwa taarifa za ziara hiyo wiki tatu zilizopita.
“Au mnataka aje nani kuukagua mradi huu ndio mjipange? Ziara zote za viongozi maelezo mnayotoa ni hayo hayo na mnapoambiwa taarifa inayohitajika mnasema mnaiandaa, tuwape muda gani iweze kukamilika ili tuipate? Alihoji Mheshimiwa H
Mheshimiwa Hapi ameitaka VETA Musoma kutekeleza agizo la Mkuu wa Wilaya ya Butiama la kumtumia mtaalamu waUkadiriaji Majengo (Quantity Surveyor) katika mradi huo haraka iwezekanavyo.
Ameikumbusha VETA kuwa ni taasisi ya serikali na ikiwa katika Mkoa wa Mara inatakiwa kuheshimu mamlaka zilizopo katika Mkoa wa Mara katika utekelezaji wa majukumu yake.
Amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela kuhakikisha kuwa taasisi zote za serikali zilizopo katika Mkoa wa Mara zinaleta taarifa kila mwezi ili kuweza kujua shughuli wanazozifanya, miradi inayotekelezwa na serikali katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mwalimu Moses Ludovick Kaengele ameeleza kuwa VETA ilitakiwa kuleta taarifa kwenye Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Butiama na baada ya kuwasilisha kamati ilibaini mapungufu katika taarifa hiyo na kumwagiza msimamizi wa mradi huo kwenda kuirekebisha kabla ya ziara ya Mkuu wa Mkoa jambo ambalo hawakutekeleza.
“Wakati wa Mwenge wa Uhuru pia hawa waliagizwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Butiama kurekebisha taarifa yao na hawakufanya mpaka mradi huu ukakataliwa kuwekewa jiwe la msingi na Mwenge wa Uhuru 2021” alisema Mwalimu Kaengele.
Mwalimu Kaengele ameeleza kuwa huenda kuna kitu menejimenti ya VETA inakificha kutokana na masahihisho walioyokuwa wanaambiwa mara kwa mara ili kukamilisha taarifa hiyo hawafanyi.
Masahihisho ambayo walikuwa wameelezwa ni pamoja na taarifa ya matumizi ya fedha kwenye kila jengo na asilimia ya ukamilishaji wa ujenzi katika kila jengo ambapo wamekuwa hawafanyi.
Tayari mradi huo umeshatembelewa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mwenge Maalum wa Uhuru (2021)ambao ulitakiwa kuweka jiwe la msingi na Mkuu wa Mkoa wa Mara ambao wote hawajaridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na hususan taarifa za fedha na maendeleo ya mradi huo.
Aidha kwa sasa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) katika Wilaya ya Butiama inaendelea na uchunguzi wa mradi huo kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021.
Mradi wa ujenzi wa VETA Butiama unatekelezwa na VETA kupitia Chuo cha VETA Musoma ambao ndio wasimamizi wakuu wa mradi huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa