Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee leo tarehe 8 Septemba, 2022 ametoa siku saba kwa Mgodi wa Dhahabu wa CATA Mines kulipa madeni wanaoyodaiwa kwa mujibu wa sheria zinazosimamia uchimbaji wa madini hapa nchini.
Mheshimiwa Mzee ametoa muda huo baada ya kupewa taarifa kuwa mgodi huo haujalipa fedha ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) kwa mwaka 2021 na 2022 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na haujapeleka michango wa wafanyakazi katika Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kama unavyotakiwa.
“Baada ya siku saba, ninataka kupata taarifa kuwa madeni haya yote yamelipwa kwa mujibu wa sheria na kuanzia sasa Mkoa wa Mara utawasimamia kuhakikisha mnatekeleza sheria za Tanzania ikiwemo mgodi kuimarisha mahusiano na jamii inayouzunguka” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, Mheshimiwa Mzee ameutaka mgodi huo kuanza majadiliano na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kuhusiana na malipo ya fedha ya CSR kwa mwaka 2022 ili kuweza kuilipa fedha inayotakiwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mzee ameuagiza mgodi huo kupata maana sahihi ya CSR baada ya kuona taarifa yao inayoonyesha fedha walizotoa kama msaada kwa watu na makundi mbalimbali na baadhi ya matumizi ya kawaida ya uendeshaji wa mgodi yakiorodheshwa kama sehemu ya CSR jambo ambalo sio sahihi.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Mzee ameutaka mgodi huo kuchangia maendeleo ya Wilaya ya Butiama na kuahidi ataenda kukagua visima ambavyo mgodi huo umevijenga katika vijiji vinne vinavyouzunguka mgodi huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mgodi huo Bwana Mark De Beer akitoa taarifa ya mgodi huo kwa Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa mgodi huo unamilikiwa kwa ubia kati ya Mwekezaji wa Canada na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kupitia Shirika la Mzinga ambalo linamiliki asilimia 10 ya hisa za Kampuni hiyo.
Bwana De Beer ameeleza kuwa uzalishaji katika mgodi huo ulianza mwaka 2016 hata hivyo mwaka 2017 ulisimama na baadaye kuanza tena mwaka 2018 na unaendelea mpaka sasa uzalishaji katika mgodi unaendelea vizuri.
“Kwa sasa tunashukuru sana mgodi umeunganishwa kwenye umeme wa gridi ya taifa wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) na hii imetusaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji katika mgodi wa CATA Mines.
Aidha, Bwana De Beer ameeleza kuwa wanaendelea kulipa fidia kwenye maeneo ya wananchi baada ya maeneo hayo kufanyiwa tathmini na kufanya makubalianao na wananchi wanaouzunguka mgodi huo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa amezungumza na Menejimenti ya Mgodi huo, kupokea taarifa ya maendeleo ya mgodi na kukagua maeneo mbalimbali ya mgodi huo.
Mheshimiwa Mzee aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Butiama na maafisa wengine kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi za Madini na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa