Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo (tarehe 23 Septemba, 2023) amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na ametoa siku 20 kwa Halmashauri za Musoma DC na Bunda DC kuhamia kwenye majengo mapya ya Halmashauri hizo.
Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo baada ya kukagua ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Musoma linaloendelea kukamilishwa katika eneo la Suguti na kuiagiza Halmashauri hiyo kumalizia upande mmoja wa jengo hilo na kuhamia.
“Hili jengo hapa tayari limeshakaa vizuri, unahitajika ukamilishaji wa mambo yaliyobakia na usafi tu jengo lianze kutumika” amesema Mhe. Mtanda.
Aidha, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha mawasiliano yanaimarishwa katika jengo hilo ili kuwezesha mifumo yote na wataalamu wote wa Halmashauri hiyo kuhamia katika eneo la Suguti ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Mtanda amewataka wananchi wa eneo la Suguti kuandaa sherehe ya kuipokea Halmashauri yao katika eneo la Suguti na kuitaka Halmashauri hiyo kuhakikisha inahamia katika muda iliyopewa.
Akiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Mhe. Mtanda amemuagiza Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Miundombinu na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Musoma kuandaa taarifa ya kiasi cha fedha kinachohitajika ili huduma muhimu ziweze kuongezwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Aidha, Mheshimiwa Mtanda ametoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kupeleka shilingi milioni 41 ili kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Kiriba ili huduma ziweze kuanza katika kituo hicho.
Mhe. Mtanda amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Manyere kwa kujitolea kusaidia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Manyere kwa kusaidia kusogeza viashiria kama vile mchanga, mawe na kokoto katika eneo la ujenzi wa mradi huo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara amekagua ujenzi wa nyumba mbili za walimu (two in one) katika Shule ya Sekondali ya Ifulifu, ujenzi wa Kituo cha Afya Kiriba na ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Wanyere.
Aidha,Mkuu wa Mkoa amekagua ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, kutembelea ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na kukagua huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Kamati ya Siasa ya Wilaya, Kamati ya Ulinzi ya Wilaya, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii, wawakilishi wa Makatibu Tawala wasaidizi sehemu za Elimu na Miundombinu na viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa