Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 28 Julai, 2025 amefanya ziara Wilaya ya Tarime na kumtaka Mkuu wa Wilaya ya Tarime kuhakikisha wanafunzi wote wa Shule ya Sekondari ya J. K. Nyerere iliyopo Nyamwaga, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wanapata chakula cha mchana wakiwa shuleni.
Mhe. Mtambi ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wanafunzi wa kidato cha pili wa shule hiyo baada ya kupokea taarifa kuwa wanafunzi wanaosoma kutwa wa kidato cha kwanza hadi cha nne ambao wazazi wao wamechangia chakula tu ndio wanaopewa chakula shuleni.
“Ninatoa siku 14 Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Tarime hakikisha wanafunzi wote wa shule hii ikiwemo na hawa wanaosoma kutwa wanapata chakula cha mchana wakiwa shuleni, hali hii haikubaliki” amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, Mhe. Mtambi amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wote wa kidato cha pili wa shule hiyo wanaoendelea na mtihani wa upimaji wa kidato cha pili Kimkoa ulioanza leo katika Mkoa wa Mara.
“Mkurugenzi wapatie chakula cha mchana hawa wanafunzi wanaofanya mtihani mpaka mtihani wao utakapoisha ili waweze kufanya vizuri katika mtihani wao” ameagiza Mhe. Mtambi.
Akizungumza katika eneo hilo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya J. K. Nyerere Mwalimu Melesiana Julius Gerald amesema kuwa uongozi wa shule pamoja na Halmashauri hiyo umefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wanafunzi wote wanapata chakula shuleni.
Mwalimu Gerald amesema kwa sasa wanafunzi wote wa kidato cha tano na sita ambao wanakaa bwenini wanapata chakula hata hivyo baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne wanaosoma kutwa katika shule hiyo hawapati chakula shuleni.
“Kwa sasa ni kama robo tatu ya wanafunzi wanaosoma ndio wanapata chakula shuleni na wengine hawapati chakula kutokana na ugumu wa wazazi kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao” amesema Mwalimu Gerald.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amekabidhi mizinga ya kufugia nyuki 121 iliyotolewa na wadau mbalimbali kwa Baraza la Wazee pamoja na wazee wa mila wa koo 12 za Kabila la Wakurya wa Wilaya ya Tarime na kuwahakikishia wazee kuwa Serikali inauthamini sana mchango wao katika jamii.
Akizungumza katika tukio hilo, Mhe. Mtambi amesema lengo la kuwapa mizinga hiyo ni kuanzisha miradi wa ufugaji nyuki katika misitu iliyopo katika Wilaya ya Tarime jambo ambalo litawaweka wazee hao kuwa karibu na misitu ambayo wamekuwa wakiitunza katika maisha yao yote.
Mhe. Mtambi ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wazee hao kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa kupiga kura na kuihamasisha jamii kupiga kura ili kupata haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi watakaowaongoza katika nafasi mbalibmbali ikiwemo Rais, Wabunge na Madiwani.
Kanali Mtambi amewashukuru wadau wote waliochangia kufanikisha wazee hao kupata mizinga ya kufugia nyuki ambayo itawasaidia kuanzisha mradi wa kuwainua kiuchumi na kuwaeleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wazee.
Aidha, Mhe. Mtambi ambaye katika ziara hiyo ameambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa na Kamati ya Wataalamu wamekagua miradi itakayotembelewa na Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa mwaka 2025.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa