Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ndani ya miezi miwili ili iweze kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Hapi ametoa maagizo haya leo tarehe 4 Agosti 2021 wakati alipofanya ziara katika halmashauri hiyo kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
“Haiwezekani wataalamu mmekaa tu fedha inakuja mpaka inarudi bila kufanyiwa kitu chochote kile, sasa naagiza hadi kufikia mwishoni mwa Desemba 2021 hospitali hii iwe inatumika na hatutakubali tena visingizio,” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Musoma kuhakikisha ujenzi wa wodi tatu za wagonjwa katika hospitali hiyo ambayo imeletewa fedha miezi sita iliyopita unaanza na unakamilika kwa haraka.
Mheshimiwa Hapi ameitaka SUMA JKT inayojenga mradi wa ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi hiyo kwa mujibu wa mkataba.
Awali wakitoa taarifa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wlaya ya Musoma Bwana Frank Magabiro pamoja na Mhandisi wa wilaya Gibai James Maige wameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Hata hivyo mradi huo haukukamilika kwa sababu fedha zake baada ya muda wa matumizi kuisha zilirudishwa serikalini, baadaye zikaletwa tena Mei, 2021 lakini hadi tarehe 30 Juni 2021 fedha hizo hazikutumika zikarudi tena serikalini.
Aidha walieleza kuwa kwa sasa fedha hizo zimeletwa tena na wapo katika mchakato wa kununua vifaa na kuleta maji eneo la ujenzi ili kukamilisha ujenzi huo.
Wakati huo huo hospitali hiyo ilipokea fedha za ujenzi wa wodi tatu za wagonjwa lakini halmashauri imenunua baadhi ya vifaa vya ujenzi na kufyatua matofali lakini ujenzi haujaanza.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Hapi pia alitembelea mradi wa ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya wilaya ya Musoma, miradi ya Shule ya Sekondari ya Msihakamano, Sekondari ya Ufundi ya Musoma na Bandari ya Musoma inayomilikiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Hapi aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Alfany Haule, mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma na viongozi wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa