Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo tarehe 7 Septemba 2022 ametembelea Mgodi wa Dhahabu wa Matongo yaani Matongo Gold Mines uliopo katika eneo la Nyamongo katika Wilaya ya Tarime.
Akiwa katika Mgodi huo, Mheshimiwa Mzee alipokea taarifa ya maendeleo ya mgodi huo na kukagua eneo la mgodi huo na kuwashauri kuhusu namna bora ya kuanza uchimbaji katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mzee amewataka wawekezaji wa mgodi huo kutoa taarifa kama watakwama katika kukamilisha upatikanaji wa vibali muhimu ili uchimbaji wa madini katika mgodi huo uweze kuanza kwa haraka.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mgodi wa Dhahabu wa Matongo Bwana William Samson ameeleza kuwa mgodi huo ulianza mwaka 2019 baada ya kupatiwa lesseni 10 za uchimbaji mdogo kwa jina la mtu binafsi baadaye iliundwa kampuni na kubadilisha umiliki wa lesseni hizo kuwa wa kampuni.
Bwana Samson ameeleza kuwa mpaka sasa mgodi huo haujaanza uchimbaji ukisubiria vibali kutoka Baraza la Taifa la Mzingira (NEMC) kilichoombwa hivi karibuni na mitambo kutoka kwa mbia wao nje ya nchi.
Ameeleza kuwa tayari mgodi huo umeanza kulipa fidia kwa wananchi waliokuwepo katika eneo hilo ambapo watu 30 waliokuwa na nyumba, mashamba au viwanja wameshalipwa zaidi ya shilingi milioni 300.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara na maafisa wengine kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa