Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee leo ametembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa katika eneo la Mwitongo Wilayani Butiama na kuzungumza na familia ya Baba wa Taif ana Wazee wa Wilaya ya Butiama na kuzulu kaburi la Baba wa Taifa pamoja na kupata historia na kumbukumbu mbalimbali za eneo hilo.
Baada ya kuwasili Mkuu wa Mkoa alipokelewa na wanafamilia wakiongozwa na Mheshimiwa Peter Wanzagi Nyerere ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama pamoja na wanafamilia wengine.
Aidha, katika eneo hilo Mkuu wa Mkoa alikutana na Kamati ya Wazee wa Wilaya ya Butiama wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bwana Richard Kibiriti na kuiahidi kuwa atapanga ziara maalum kwa ajili ya kuzungumza nao kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimaendeleo kwa Wilaya ya Butiama.
Katika eneo hilo, Mheshimiwa Mzee pia alitembelea kaburi la Baba wa Taifa na kuweka mashada na kuomba dua iliyoongozwa na viongozi wa dini.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa pia alionyenyeshwa Mwenge wa Mwitongo uliopo Nyumbani kwa Baba wa Taifa pamoja na kupewa historia ya Mwenge huo na umuhimu wake katika historia ya Tanzania.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alitembelea pia nyumba za Mwalimu, makaburi ya wazazi na ndugu yaliyopo eneo hilo pamoja na nyumba ya zamani ya Mwalimu Nyerere na Baba yake Chiefu Burito Nyerere.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu, Viongozi wa Wilaya na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa