Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameanza ziara yake katika Wilaya ya Serengeti ambapo ametatua mgogoro wa mpaka katika Kijiji cha Rigicha na kuwapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo kwa kufuata sheria na taratibu.
Akizungumza katika eneo hilo, Mhe. Mtambi amesema wananchi hao wamekuwa ni mfano wa kuigwa katika utatuzi wa migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Mara kwa kufuata sheria na maridhiano ya kifamilia na kijamii.
“Ninaomba niwapongeze sana wananchi wa Kijiji cha Rigicha, kwa busara na ustahimilivu wenu wa kusubiri kuutatua mgogoro huu kwa kufuata misingi ya haki na sheria, hongereni sana” amesema Mhe. Mtambi.
Baada ya kuwasili katika eneo hilo, Mkuu wa Mkoa amewasikiliza wananchi kutoka familia moja ambao walikuwa wanagombea mpaka wa eneo pamoja na maombi ya kuhamisha njia ya muda mrefu ili kuruhusu shamba la familia kuwekewa mipaka.
Mgogoro huo ulitokana na Bi. Magdalena Francis kuomba kuhamisha barabara ya eneo hilo ipite pembezoni ya shamba la familia yake na baadaye kuanzisha mgogoro na Bwana Mgosi Magesa ambaye anapakana naye na kugombea sehemu ya shamba hilo.
Hata hivyo, Mhe. Mtambi amesuluhisha mgogoro huo na kusimamia uwekaji wa mpaka mpya wa barabara katika eneo hilo na kuwataka familia iliyokuwa na mgogoro kushikana mikono kuashiria kuhitimishwa rasmi kwa mgogoro huo.
Baada ya hapo, Mhe. Mtambi amezungumza na wananchi wa Kijiji hicho na kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri kuongeza watumishi katika Zahanati ya Kijiji cha Rigachi na kuitaka RUWASA kukamilisha mradi wa maji katika eneo hilo.
Kwa upande wake kiongozi wa familia iliyokuwa na mgogoro wa ardhi Bwana John Francis Kisongo alisema kuwa eneo hilo ni la familia yao na mababu zao walikuwa wanalima wa mashamba hayo wakati wakiwa hai na wanaogombania sasa ni warithi baada ya wamiliki wa awali kufariki.
Bwana Kisongo amewataka wanafamilia hao kuheshimu mpaka uliowekwa leo katika eneo hilo na kuwaomba kuendelea kuishi kwa amani kama ilivyokuwa awali kabla ya kuanza kwa mgogoro huo.
Baada ya hapo, Mkuu wa Mkoa amekagua mradi wa Maji wa Nyiberekela na kufanya kikao cha ndani na viongozi wa Wilaya ya Serengeti kabla ya kufanya mkutano wa hadhara katika eneo la Isenyi, Kata ya Isenyi na kupokea na kutatua kero mbalimbali za wananchi wa eneo hilo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara aliambatana na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti, Mwenyekiti wa Halmashauri na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Wakuu wa Taasisi za umma zilizopo Wilaya ya Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa