Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo ametoa taarifa ya ziara ya Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 25 Februari, 2025 hadi tarehe 29 Februari, 2024.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Mhe. Mtanda amesema katika ziara hiyo, Mhe. Waziri Mkuu anategemea kuzungumza na watumishi na viongozi, kufanya mikutano ya hadhara, kutembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya Maendeleo katika sekata za Utawala, Elimu, Afya na miundombinu.
“Maandalizi ya ziara ya Mhe. Waziri Mkuu katika Mkoa wa Mara yamekamilika. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wananchi, watumishi na viongozi wa ngazi mbalimbali walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha maandalizi ya ziara ya Mhe. Waziri Mkuu katika Mkoa wa Mara” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda amesema mapokezi ya Mhe. Waziri Mkuu kimkoa yatafanyika eneo la Ndabaka, Wilaya ya Bunda tarehe 25 Februari, 2024 mchana na baadaye ataelekea Ukumbi wa Uwekezaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa ajili ya kupokea taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa tarehe 26 Februari, 2024 Mhe. Waziri Mkuu atasalimia wananchi eneo la Mariwanda kabla ya kutembelea na kukagua Shule ya Msingi Sabasita iliyopo eneo hilo, atakagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Mara Halmashauri ya Wilaya ya Bunda. Baada ya hapo Mhe. Waziri Mkuu atakagua na kuzindua mradi wa maji wa Sazira na kufanya kikao na watumishi na viongozi kisha kufanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Msingi Miembeni, Bunda Mjini.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa tarehe 27 Januari, 2024 Mhe. Waziri Mkuu atakagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, kufanya kikao na watumishi na viongozi, kuwasalimia wananchi wa Butiama na kutembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere eneo la Mwitongo, Butiama.
Aidha, Mhe. Waziri Mkuu atafanya kikao na watumishi na viongozi Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Sokoine, Mugumu na baadaye kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Getarungu. Mheshimiwa Waziri Mkuu ataelekea Nyamwaga ambapo ataweka jiwe la msingi katika jengo la utawala Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na kusalimiana na wananchi.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa tarehe 28 Feburuari, 2024 Mhe. Waziri Mkuu atatembelea na kukagua mradi wa maji Komuge na baadaye kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kabla ya kufanya mkutano wa hadhara katika eneo la Utegi. Baadaye Mhe. Waziri Mkuu atafanya mkutano wa hadhara katika eneo la Sirari na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa soko la kimkakati la Mji wa Tarime na kufanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Serengeti katika Mji wa Tarime.
Tarehe 29 Februari, 2024 Mhe. Waziri Mkuu atakagua ujenzi wa Uwanja wa Ndege Musoma ataelekea kijiji cha Suguti kuweka jiwe la msingi katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na atazungumza na viongozi na watumishi.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Mhe. Waziri Mkuu ataenda kijiji cha Bwai (Bwai Kumsoma) kwa ajili ya kuzungumza na wananchi katika uwanja katika Kijiji cha Bwai na kuhitimisha ziara yake katika Manispaa ya Musoma ambapo atafanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Sekondari Mara.
Mhe. Mtanda amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mapokezi na mikutano ya hadhara iliyopangwa karibu na maeneo yao.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa