HAPI ATAKA WANANCHI KULINDA MIRADI YA MAJI
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhehsimiwa Ally Salum Hapi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kulinda miundombinu na vyanzo vya maji ili miradi ya maji inayoletwa na serikali katika maeneo yao iweze kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
Hayo yameelezwa katika ziara yake aliyoifanya katika Mji wa Shirati katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kukagua mradi wa Maji unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA).
“Mradi ya maji kama hii inaletwa kwa lengo la kutatua tatizo kubwa la maji ambalo lilikuwepo na linawaathiri kwa kiasi kikubwa wanawake wanaotumia muda mwingi kutafuta maji” alisema Mheshimiwa Hapi.
Amewatahadharisha wanaohujumu miundombinu ya maji kuwa serikali haitawafumbia macho kuona wananchi wengi wanataabika kwa sababu ya watu wachache wanaohujumu kwa manufaa yao.
Mkuu wa Mkoa amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kipolisi Shirati kuwatafuta watu waliohujumu bomba la mradi wa maji Shirati tarehe 11 Julai 2021 na kusababisha hasara kwa serikali na wananchi wa Mji wa Shirati kukosa huduma ya maji.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Hapi alitoa ofa kwa wananchi wa Mji wa Shirati kuunganishiwa huduma ya maji majumbani kwa mkopo baada ya kulipia nusu ya gharama inayohitajika kuunganisha maji.
“Ninatoa ofa kuanzia sasa mtu yeyote atakayehitaji kuunganishiwa maji anaweza kujiandikisha na kulipa nusu ya gharama ya kuunganishiwa maji na ataunganishiwa maji kwa mkopo kuanzia tarehe 01 Agosti 2021” alisema Mheshimiwa Hapi.
Amewahamasisha wanaume kuchukua fursa hiyo kuunganisha maji kwa ajili ya familia zao ili kuwaacha wanawake waendelee kufanya shughuli nyingine za kiuchumi.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa miundombinu ya maji wa Shirati, Mkurugenzi wa MUWASA CPA Joyce Msiru ameeleza kuwa watu wasiojulikana walikata bomba la mradi huo lenye ukubwa wa nchi tisa na kusababisha shida ya maji kwa wakazi wa Mji wa Shirati.
Hata hivyo Bibi Msiru ameeleza kuwa kwa sasa bomba hilo limetengenezwa na upatikanaji wa maji umerejea katika hali yake ya kawaida baada ya bomba lililokatwa kutengenezwa.
“Kwa sasa huduma ya maji inapatikana kwa asilimia 20 ya wakazi wote wa Mji wa Shirati na mpaka sasa jumla ya wateja 494 wameshaunganishiwa maji majumbani na wengine waliobakia wanachota maji kwenye vioski vya maji” alisema CPA Msiru.
Bibi Msiru ameeleza kuwa MUWASA imepewa jukumu la kusimamia mradi huo kufuatia ziara ya Waziri wa Maji aliyoifanya katika Wilaya ya Rorya Tarehe 6 Januari 2021 baada ya Mji wa Shirati kukosa maji kuanzia mwaka 2015 baada ya kuharibika kwa mradi uliokuwepo.
Ameeleza kuwa baada ya mradi wa ukarabati kukamilika, Wizara ya Maji ilikabidhi mradi huo kwa MUWASA kwa ajili ya kuuendesha kwa muda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Mheshimiwa Samweli Kiboye maarufu kama Namba 3 akizungumza katika mkutano wa wananchi amemuaomba Mkuu wa Mkoa kufuatilia suala la kuanzisha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Shirati.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa hapa wananchi hawa kilio chao cha muda mrefu ni kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Shirati, wananchi wanatamani sana kuanzishwa kwa mamlaka hiyo” alisema Mheshimiwa Kiboye.
Ameeleza kuwa kwa sasa Mji wa Shirati unawakazi wengi sana wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela; Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara na Wilaya ya Rorya, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Katibu Tawala wa Wilaya ya Rorya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya na viongozi wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa