Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee amewaomba wadau wa maendeleo na watu wenye uwezo kuzisaidia Nyumba Salama, vituo vinavyowahudumia watoto waliokimbia vitendo vya ukatili katika jamii ili kuviwezesha vituo hivyo kuwahudumia watoto kwa ufanisi na kuepusha watoto kurudi tena kwenye ukatili.
Mheshimiwa Mzee ametoa wito huo baada ya kupokea taarifa kuwa watoto 70 ambao walikuwa wamekimbilia Nyumba Salama ya AFTGM Masanga iliyopo katika Wilaya ya Tarime wamekeketwa baada ya kurejeshwa majumbani kwao baada ya msimu wa ukeketaji kuisha.
“Hili linatokea kwa sababu hivi vituo havina uwezo wa kutunza watoto wengi kwa muda mrefu na kulazimika kuwarejesha kwa wazazi ambao wanaenda kuwakeketa hata baada ya kuingia makubaliano na vituo hivyo kuwa watawalinda” alisema Mzee.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa namna bora ya kuwaepusha watoto kukumbana na ukatili huo ni kuziwezesha Nyumba Salama ili ziweze kutoa huduma kwa muda mrefu zaidi hata baada ya muda wa ukeketaji kuisha.
Mheshimiwa Mzee amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara itatoa shilingi milioni 9 kusaidia Kituo cha AFTGM Masanga, Shirika la Hope for Women and Girls lenye Nyumba Salama mbili za Matumaini katika Wilaya za Butiama na Serengeti na Nyumba Salama ya Kanisa la Anglican Tanzania (ACT Mara).
Aidha, katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliitisha harambee na kufanikiwa kukusanya mchango zaidi ya shilingi 200,000 kutoka kwa viongozi alioambatana nao na kuukabidhi kwa Msimamizi wa Kituo cha ACT Mara.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Women and Girls Bibi Rhobi Samwel ameeleza kuwa katika kuwatunza watoto wanakutana na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya viongozi wa siasa kuwasaidia watu waliokamatwa kwa makosa ya ukeketaji ili waachiwe.
Bibi Rhobi Samwel amepongeza ushirikiano wanaoupata kutoka kwa viongozi mbalimbali wa Serikali katika mapambano dhidi ya ukeketaji na vitendo vingine vya ukatili ikiwemo ndoa za utotoni, vipigo, na ukeketaji.
Kwa sasa Mkoa wa Mara una Nyumba Salama za kuwahifadhi waliokimbia ukatili nne ambazo ni AFTGM Masanga (Tarime), ACT Mara (Serengeti), Matumaini (Serengeti na Butiama).
Hata hivyo, kutokana na changamoto ya fedha, watumishi, sehemu ya kuishi watoto wengi wanaopokelewa katika vituo hivi hurudishwa baada ya msimu wa ukeketaji kuisha (Agosti- Desemba) hata hivyo kwa mwaka huu ukeketataji unaendelea kufanyika kwa watoto waliokuwa wamekimbia awali.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Mkoa, Kamati ya Usalama ya Wilaya za Tarime, Serengeti na Butiama, baadhi ya maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Menejimenti za Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Serengeti na Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa