Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Mungiya Mzee leo ameongoza kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai-Desemba, 2022 na kuwataka viongozi na watendaji wa Serikali kusimamia kwa weledi utekelezaji wa afua za lishe kwenye maeneo yao.
Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Mzee amewataka viongozi kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani ili Halmashauri ziweze kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya masuala ya lishe na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika utekelezaji wa mkataba wa lishe na kuepuka kuwa sehemu ya kuchochea changamoto hizo.
“Viongozi tujitahidi kuhakikisha tunatekeleza Maagizo ya Serikali kuhusu mkataba wa lishe na kuacha kutoa visingizio mbalimbali kwa nini mkataba huo hautekelezeki” amesema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee amesema wanafunzi kula shuleni ni Maagizo ya Serikali, Wilaya na Halmashauri zihakikishe kuwa watoto wanapata angalau mlo mmoja shuleni kila siku ili kuwafanya wasome kwa ufanisi.
Aidha, Mheshimiwa Mzee amesema ataendelea kuchukua hatua kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na viongozi wengine wote watakaokwamisha utekelezaji wa mkataba wa lishe katika maeneo yao bila sababu za msingi.
Mheshimiwa Mzee amesema hatakubali kuona Mkoa wa Mara unaendelea kuwa wa mwisho katika upimaji wa utekelezaji wa afua za lishe Kitaifa kutokana na uzembe wa viongozi na watendaji wenye dhamana ya kufanya hivyo.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amewataka Wakuu wa Wilaya kuwasimamia watendaji wa Halmashauri zilizopo chini yao kuhakikisha chakula kinatolewa katika shule zote za msingi na sekondari ili watoto waweze kujifunza kwa ufanisi wakati wa masomo.
“Pamoja na kuwa kuna changamoto ya wazazi kutopenda kuchangia chakula au kutotaka watoto wao kula nje ya nyumba zao, viongozi mpo, tuwaelimishe hawa wazazi, inawezekana” amesema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, ameagiza shule zote katika Mkoa wa Mara kuacha mara moja utaratibu wa kuwaruhusu wauzaji wa vitu mbalimbali na badala yake kila shule iwe na jiko la kupika chakula cha wanafunzi ili kulinda afya za wanafunzi na walimu katika maeneo hayo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu ameeleza kuwa kuwapa wanafunzi chakula wakiwa shuleni ni muhimu kwani linamanufaa makubwa katika ufundishaji na ujifunzaji wa watoto.
“Maeneo mengi imebainika kuwa wanafunzi wakipewa chakula hata mahudhurio ya watoto darasani yanaongezeka na wanaweza kusoma kwa ufanisi kuliko wakisoma na njaa” alisema Dkt. Masatu.
Aidha, alifafanua kuwa mwongozo wa chakula shuleni ni wa kitaifa na unatekelezwa na Halmashauri zote hapa nchini na katika Mkoa wa Njombe shule zote za msingi na sekondari wanatoa chakula na matokeo ya mitihani ya Kitaifa Mkoa huo unafanya vizuri na moja ya sababu ni kuwa wanafunzi wanapata chakula shuleni.
Kikao cha tathmini ya lishe kimkoa kilihudhuriwa pia na Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Idara na Vitengo vilivyopo ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Idara za Fedha, Mipango, Utawala na Rasilimali Watu, Waganga Wakuu wa Halmashauri na Maafisa Lishe.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa