Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Meja Jenerali Suleiman Mzee leo tarehe 6 Agosti, 2022 amewasili katika Mkoa wa Mara na kuwataka viongozi wa Mkoa huo kushirikiana katika kuleta mabadiliko ya kimaendeleo na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza baada ya mapokezi yake yaliyofanyika leo baada ya kuwasili, Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa viongozi wa Mkoa wa Mara wakishirikiana vizuri wananchi watapata maendeleo kwa haraka zaidi.
“Mimi nitajitahidi kuwa mvumilivu maana Mheshimiwa Rais (Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) alisema huku ni uraiani, lakini sitakuwa mvumilivu na mtu yoyote anayekwamisha au anayechelewesha miradi ya maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Mara” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee amewaomba viongozi wa Mkoa wa Mara kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
“Hapa tupo kwenye ziwa, kilimo chetu bado kinategemea mvua, lakini tukishirikiana tutatafuta ufumbuzi wa kuweza kutumia maji ya ziwa katika kilimo cha umwagiliaji na kuwasaidia zaidi wakulima” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, Mheshimiwa Mzee amewataka viongozi kushiriki kikamilifu katika maandalizi na uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ili Mkoa wa Mara uweze kufanya vizuri katika zoezi hilo kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Mimi ninawaomba tushirikiane vizuri katika maandalizi na hususan uhamasishaji wa wananchi katika kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ili Sensa ya mwaka huu ifanyike vizuri katika Mkoa wetu” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mkuu wa Mkoa amepokelewa na viongozi wa Mkoa wa Mara wakiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu katika eneo la Ndabaka, Wilaya ya Bunda ambapo ni mpakani kati ya Mkoa wa Mara na Mkoa wa Simiyu katika Barabara ya Mwanza- Musoma- Sirari.
Baada ya mapokezi hayo, viongozi hao walielekea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara ambapo Mkuu wa Mkoa alisaini kitabu na kuzungumza na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mara walioshiriki mapokezi hayo.
Viongozi wengine waliokuwepo katika mapokezi hayo ni Wakuu wa Wilaya, Kamati ya Usalama ya Mkoa, baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Wakuu wa Idara na Vitengo vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala wa Wilaya na baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Meja Jenerali Suleiman Mzee ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara tarehe 31 Agosti, 2022 kuchukua nafasi ya Mheshimiwa Dkt. Raphael Chegeni aliyeteuliwa tarehe 28 Agosti, 2022 kuchukua nafasi ya Mheshimiwa Ally Salum Hapi ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa