Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kuimarisha Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani ili kuweza kumsaidia Mkurugenzi kuisimamia halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa ametoa agizo hilo leo tarehe 14 Julai, 2022 katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka wa fedha 2020/2021.
“Hiki kitengo kwa sasa kina mtumishi mmoja tu, hakina gari la kufanyia shughuli za kitengo hicho hivyo kama CAG alivyoelekeza, kitengo hiki kiimarishwe haraka” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha ameagiza kuongeza watumishi katika Kitengo cha Manunuzi ambacho ikama inataka kiwe na watumishi 6 lakini kwa sasa kitengo hicho kina watumishi wa wawili tu.
Mheshimiwa Hapi ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kukusanya kwa asilimia 105 ya mapato ya ndani katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 pamoja na kupata hati safi katika ukaguzi wa mwaka wa fedha 2020/2021.
Aidha ameitaka Halmashauri hiyo kukamilisha miradi yote ya muda mrefu kabla ya kuanzisha miradi mipya ili kuleta matumaini kwa wananchi wa Halmashauri hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bwana Emanuel Mkongo ameeleza kuwa katika ukaguzi wa CAG kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Halmashauri imepata hati safi.
Hata hivyo Bwana Mkongo ameeleza kuwa Halmashauri hiyo ilikuwa na hoja za miaka ya nyuma 22 kati ya hizo hoja 09 zimehakikiwa na kufungwa, hoja 05 zinajirudia rudia, hoja 08 zipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
Bwana Mkongo ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri ilikuwa na hoja 28, kati ya hoja hizo 12 zimefungwa, hoja 02 zimepitwa na wakati na hoja 14 zipo kwenye hatua za utekelezaji.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa