Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo tarehe 12 Oktoba, 2022 amefanya kikao na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na baadhi ya Wakuu wa Idara za Halmashauri kwa lengo la kutoa maelekezo kuhusiana na masuala mbalimbali.
Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Mzee amewataka viongozi wa Wilaya kuzisimamia Halmashauri zao ili pesa za ujenzi wa vyumba vya madarasa zilizopokelewa ziweze kujenga vyumba hivyo kwa ubora na kwa wakati.
“Mimi ninatoa siku 60 tu vyumba vya madarasa viwe vimekamilika na nitakapokuja kukagua nitagombana na viongozi kama mambo hayajaenda vizuri sio watendaji wa chini” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee amewataka viongozi wa Wilaya na Halmashauri kutimiza wajibu wao kwa Taifa na wananchi wa Mkoa wa Mara ili kuleta matokeo yanayohitajika na sio kusubiri kusukumana.
Akitoa taarifa katika mkutano huo, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi, Elimu Bwana Ahidi Jailosi Sinene ameeleza kuwa Mkoa wa Mara umepokea jumla ya shilingi bilioni 10.920 katika akaunti za shule 144 za Sekondari kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa 546.
Bwana Sinene ameeleza kuwa ujenzi wa vyumba vya madarasa hayo ni sehemu ya matayarisho ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza Januari, 2023.
Katika mgao wa vyumba hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti imepata vyumba 58 (1,160,000,000), Halmashauri ya Mji wa Bunda vyumba 77 (1,540,000,000), Halmashauri ya Wilaya ya Bunda vyumba 102 (2,040,000,000) na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama vyumba 77 (1,540,000,000).
Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime vyumba 23 (460,000,000), Halmashauri ya Mji wa Tarime vyumba 41 (820,000,000), Halmashauri ya Wilaya ya Rorya vyumba 66 (1,320,000,000), Manispaa ya Musoma vyumba 67 (1,340,000,000) na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma vyumba 35 (700,000,000).
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa