Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo ametembelea mradi wa Maji wa Mugango- Kiabakari- Butiama na kumtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mugango -Kiabakari (MKWSSA) kuwasilisha mpangokazi wa ukamilishaji wa mradi huo ofisini kwake tarehe 30 Desemba, 2022.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa hajaridhiwa na utekelezwaji wa mradi huo ambao awali ulitakiwa ukamilike Desemba 17, 2022 na sasa umeongezewa muda hadi Juni, 2023.
“Tatizo ninaloliona hapa ni Mshauri Mwelekezi wa mradi anaukwamisha mradi kwa kutokujibu mapendekezo ya mkandarasi kwa wakati na kushindwa kuridhia au kukataa kuendelea na hatua inayofuata ya ujenzi, matokeo yake kazi kubwa imekwama” amesema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee amemtaka Mkurugenzi wa MKWSSA kuifahamisha Wizara ya Maji kuhusiana na mapungufu ya Mshauri Mwelekezi wa mradi ili kama inawezekana Wizara isitishe mkataba wake ili mradi uweze kukamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Mzee pia ameelezea wasiwasi wake kuhusiana na malipo ya ziada ambayo mkandarasi anaweza kuja kuidai Serikali baada ya kucheleweshwa kufanyakazi na Mshauri Mwelekezi wa mradi kwa mujibu ya mkataba.
Mkuu wa Mkoa ameahidi kuufuatilia mradi huo mara kwa mara kuanzia sasa ili wananchi wa Wilaya za Musoma na Butiama wanaotarajiwa kunufaika na mradi huo waweze kupata maji safi na salama ya uhakika.
Akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Jumanne Sagini amememshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufanya ziara katika mradi huo na kueleza kuwa katika ziara yake ya Mkoa wa Mara amepanga kuutembelea mradi huo.
“Kumekuwa na changamoto kubwa ya maji kwa wananchi wa Butiama baada ya mradi wa zamani kukatiwa maji baada ya mamlaka hiyo kukatiwa umeme na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) alisema Mheshimiwa Sagini.
Mheshimiwa Sagini ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Butiama ameahidi kuwasiliana na Wizara ya Maji ili kuweza kutatua changamoto za maji kwa wananchi wa Butiama baada ya wananchi wa eneo hilo kukosa maji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MKWSSA Mhandisi Cosmas Sanga ameeleza kuwa mradi wa maji wa Mugango- Kiabakari Butiama una thamani ya shilingi bilioni 70.5 na unajengwa na mkandarasi UNIK Construction Engineering na Mshauri Mwelekezi ni Sajdi Consulting Engineering Center.
Mhandisi Sanga ameeleza kuwa kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 71 ya utekelezaji wakati malipo katika mradi huo yamefikia asilimia 58 ya fedha zote.
“Mradi huu ulianza tarehe 17 Desemba, 2020 na ulipaswa kukamilika tarehe 17 Desemba, 2022 lakini kutokana na changamoto ya UVIKO 19 mkandarasi ameomba kuongezewa muda wa miezi sita za utekelezaji wa mradi hadi tarehe 30 Juni, 2023” alisema Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga ameeleza kuwa mradi huo kwa awamu ya kwanza unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji, chujio la maji, jengo la utawala la MKWSSA, nyumba za watumishi, matanki ya maji 7 mapya na ukarabati wa matanki mawili, usafirishaji wa maji na usambazaji wa maji kwa wananchi wa vijiji 16.
Kwa mujibu wa Mhandisi sanga, vijiji vingine 23 vitakavyonufaika na mradi huo mchakato wa zabuni kumpata mkandarasi unaendelea kupitia Wizara ya Maji.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa