Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee amekitaka Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) 822 Rwamkoma kusaidia katika kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii katika Wilaya ya Butiama.
Mheshimiwa Mzee ametoa rai hiyo wakati alipokitembelea kikosi hicho kwa ajili ya kufunga mafunzo ya vijana 891 waliopata mafunzo kwa mujibu wa sheria katika operesheni ya Jenerali Venance Mabeyo, 2022.
“Katika Wilaya ya Butiama hamna sehemu nzuri ya watu kupumzika na kupata huduma za chakula na vinywaji kwa hadhi ya wageni wa kitaifa na kimataifa wanayoitembelea Butiama, hivyo mkiboresha huduma watu na hususan wageni watakuja” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, Mheshimiwa Mzee amekitaka kikosi hicho kuongeza biashara zake inazozifanya katika eneo hilo na kufungua kiwanda cha kutengeneza mikate, duka la mboga mboga pamoja na kufungua duka katika Mji wa Musoma ili kuuza bidhaa mbalimbali wanazozalisha.
Akiwa katika eneo hilo Mheshimiwa Mzee amefungua Bwalo la Maafisa wa Jeshi na kupanda mti wa kumbukumbu, ametembelea mashine ya kuzalisha chakula cha Samaki, kukagua gwaride la vijana na kutoa zawadi kwa vijana waliofanya vizuri katika mafunzo hayo.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Kikosi hicho Luteni Kanali Gaudensia Joseph Mapunda ameeleza kuwa mafunzo ya vijana hao yameanza tangu tarehe 27 Juni, 2022 na kuhusisha vijana 904 hata hivyo 13 hawakumaliza mafunzo kutokana na utoro.
“Kati ya vijana waliopangiwa kufanya mafunzo yao katika kikosi hicho, vijana 206 walikuwa ni wasichana huku 698 walikuwa ni wavulana”alisema Bibi Mapunda.
Luteni Kanali Mapunda ameeleza kuwa vijana hao waliohitimu mafunzo yao wamefanya mafunzo mbalimbali kwa nadharia na kwa vitendo na sasa wapo tayari kulitumikia Taifa.
Aidha, Bibi Mapunda alisema kuwa Bwalo la Maafisa wa Jeshi lililofunguliwa limegharimu zaidi ya shilingi milioni 53 na ujenzi wake umekamilika.
Ameitaja miradi mingine inayoendeshwa na kikosi hicho kuwa ni pamoja na kilimo, ufugaji wa ng’ombe na Samaki, bucha, ufugaji wa nyuki na biashara ya chakula na vinywaji katika eneo la Rwamkoma na Viwanja vya Nyakabindi, Simiyu.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa