Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo amewaongoza waombolezaji katika mazishi ya Bi. Rose Andrew Nyamwera aliyefariki katika ajali ya ndege ya Precision Air iliyoanguka katika Ziwa Victoria.
Akizungumza katika mazishi hayo yaliyofanyika katika Kijiji cha Rwangwa, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Mheshimiwa Mzee amewataka watu wote walioguswa na msiba huo kuendelea kuisaidia familia hiyo na hususan watoto wa marehemu ambao wanaumri mdogo.
“Ninawaomba tuendelee kuisaidia familia hii, hawa watoto bado ni wadogo na wanamahitaji mengi tusipotee, tuendelee kuwasaidia ili na sisi tusife tukiwa bado hai” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa amekuja katika msiba wa Bi. Rose Nyamwera kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na wananchi wote wa Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mheshimiwa Dkt. Halfany Haule ameeleza kuwa katika ajali hiyo, Mkoa wa Mara umepoteza watu wawili na kwa mapenzi ya Mungu wote wanatokea katika Wilaya ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Dkt. Haule ameeleza kuwa msiba huo ni mkubwa sana kwa wananchi wa Musoma na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na kumshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuja kushirikiana nao katika msiba huo.
Katika mazishi hayo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Musoma Vijijini, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na baadhi ya watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Wengine waliohudhuria ni pamoja na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TARURA, Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Kagera na Mkoa wa Mara, watumishi wa TARURA wa Mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara.
Marehemu Rose Nyamwera alizaliwa 13 Septemba, 1987 katika Kijiji cha Kasoma, Wilaya ya Musoma na wakati wa uhai wake alikuwa ni mtumishi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Kagera.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa