Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa utulivu wa madiwani na wataalamu wa Halmashauri hiyo jambo ambalo linachochea utekelezaji wa haraka wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali leo tarehe 13 Julai, 2022, Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa utulivu wa Halmashauri hii unasababisha iweze kupata maendeleo kwa haraka.
“Ninawapongeza sana kwa utulivu, hiyo ndio siasa safi, endeleeni kuwa wamoja na kuwasimamia wataalamu ili wafanye kazi zao kwa uadilifu” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani katika mwaka wa fedha 2021/2022 na kufikia asilimia 97 hata baada ya kuongeza lengo la makusanyo hayo katikati ya mwaka huo wa fedha.
Mheshimiwa Hapi pia ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati safi kwa miaka 07 mfululizo na kuwataka wapunguze hoja za CAG ambazo zinaweza kuzuilika.
Aidha Mheshimiwa Hapi amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kuongeza watumishi katika vitengo vya Ukaguzi wa Ndani na Manunuzi ili kuimarisha utendaji kazi wa vitengo hivyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri bibi Gimbana Emanuel Ntavyo ameeleza kuwa Halmashauri ya Mji wa Tarime ilikuwa na jumla ya hoja 47 ambapo 20 zimejibiwa na kufungwa na 27 ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Bibi Ntavyo ameeleza kuw akati ya hoja hizo, hoja za nyuma 21 ambazo kati yake 09 zimefungwa na hoja 12 zipo katika utekelezaji wakati kati ya hoja mpya 26 hoja 11 zimefungwa na hoja 15 zipo katika hatua mbalimbali katika utekelezaji.
Bibi Ntavyo ameeleza kuwa Halmashauri hiyo ilikuwa na maagizo 08 ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na kati yake agizo moja limefungwa na maagizo mengine 07 yanaendelea kutekelezwa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa