Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee leo tarehe 7 Septemba, 2022 amewapongeza wachimbaji wadogo ambao wanamiliki wa Mgodi wa Dhahabu wa Irasanilo uliopo Buhemba, katika Wilaya ya Butiama kwa kujenga Soko la Madini la Buhemba lenye thamani ya shilingi milioni 350.
Mheshimiwa Mzee alitoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kuitembelea migodi yote iliyopo katika Mkoa wa Mara na kuwataka wachimbaji hao kuendelea kuungana ili kukamilisha ujenzi wa soko hilo ambalo kwa sasa lipo katika hatua za ukamilishaji.
“Ninawapongeza sana kwa kuungana na kuweza kufanya uwekezaji mkubwa wa kujenga Soko la Dhahabu la Buhemba, hii ni hatua kubwa sana mliyoifikia kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika Mkoa wa Mara” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, Mheshimiwa Mzee amewapongeza kwa kodi na michango mbalimbali wanayoitoa kwa Serikali Kuu na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na ameahidi atahakikisha fedha yote itakayotolewa katika Halmashauri inatumika vizuri ili kuleta maendeleo katika Wilaya ya Butiama na hususan eneo la Buhemba ulipo mgodi huo.
Mheshimiwa Mzee ameuagiza uongozi wa Mgodi wa Irasanilo kuongeza Kituo cha Polisi, sehemu ya kununua mahitaji mbalimbali na huduma za kwanza katika soko hilo.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amewataka wachimbaji hao kuacha kutumia kuni katika kuchoma dhahabu na kubadilika kutumia vichomea dhahabu vya kisasa ili kutunza mazingira kwa kupunguza matumizi ya mkaa.
“Ninawaomba muongeze nguvu na kubadilisha aina hii ya uchomaji wa dhahabu ili kupata vifaa vya kisasa zaidi vya kuchomea na kwa mfumo ambao hauhatarishi mazingira ya nchi yetu” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, Mheshimiwa Mzee amewataka wachimbaji hao kubadilisha mazingira na nyumba wanazoishi katika eneo hilo kwa kujenga nyumba nzuri za kisasa katika eneo hilo ili Buhemba ikiwezekana iwe ni mji mzuri wenye wafanyabiashara wakubwa.
Mheshimiwa Mzee pia amemtaka Afisa Madini Mkoa wa Mara na wataalamu wengine kufikiria na kuwaelimisha wachimbaji hao faida za wao kuwa wachimbaji wadogo au wachimbaji wakubwa na hasara zake ili waweze kufanya maamuzi sahihi.
Akitoa taarifa ya mgodi huo, Meneja wa Irasanilo Bwana Isaya Daudi ameeleza kuwa mgodi huo unamilikiwa na wachimbaji wadogo wapatao 387 waliopewa lesseni za uchimbaji mdogo na Serikali.
Bwana Daudi ameeleza kuwa kwa mwaka 2021/2022 mgodi huo ulikuwa wa kwanza katika ulipaji wa kodi za Serikali hapa nchini kwenye kipengele cha wachimbaji wadogo.
Aidha, Bwana Daudi ameeleza kuwa kwa sasa eneo hilo lina madalali wa madini wapatao 30 ambao watapangishwa katika Soko la Buhemba pindi litakapokamilika.
Katika eneo hilo, Mkuu wa Mkoa alikagua ujenzi wa Soko la Dhahabu Buhemba, alipokea taarifa za maendeleo ya mgodi huo na kuzungumza na wachimbaji wadogo wa mgodi huo ikiwa ni pamoja na kupokea changamoto zao na kuzitolewa ufafanuzi.
Awali, Mkuu wa Mkoa alitembelea Mgodi wa ZEM ambao ni mgodi wa kati unaomilikiwa na wawekezaji wa China uliopo katika Kijiji cha Nyasiroli Wilaya ya Butiama na kupokea taarifa na kukagua shughuli za mgodi huo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Kamati Usalama ya Wilaya ya Butiama, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mara, watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa