Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo amefanya ziara katika Wilaya ya Tarime na kupokea vyumba vya madarasa 64 vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.28 kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mheshimiwa Mzee ameipongeza Wilaya ya Tarime kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa madarasa na hususan utengenezaji wa viti na meza kwa ajili ya wanafunzi.
“Ninawapongeza kwa kazi kubwa mliyoifanya katika kusimamia ujenzi wa vyumba vya madarasa na yamekamilika kwa ubora na kwa wakati” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee amewataka watendaji wa Serikali wanaosimamia utekelezaji wa miradi kusimamia utekelezaji wa miradi kwa weledi na ubora unaotakiwa na sio kulipua kazi.
Aidha, amewatahadharisha wazazi ambao hawata wapeleka watoto wao kuanza shule, serikali ya Mkoa wa Mara haitamvumilia mzazi yoyote atakayeshindwa kumpeleka mtoto shule na itamchukulia hatua za kisheria.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mbunge wa Tarime Vijijini Mheshimiwa Mwita Waitara ameeleza kuwa anaishukuru sana Serikali kwa kujenga vyumba vya madarasa na Shule mpya mbili katika jimbo lake ambazo zitapunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.
Mheshimiwa Waitara ameeleza kuwa kwa mwaka huu wanafunzi wa Kata ya Sirari wanaotarajia kuanza Kidato cha Kwanza ni zaidi ya 700 na awali walikuwa na shule moja tu Sirari Sekondari, kuongezwa kwa shule mpya katika eneo hilo kumesaidia sana.
Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo na Wilaya ya Tarime kwa ujumla.
“Jimbo hili limepata shule mbili mpya moja ya milioni 600 na nyingine ya zaidi ya bilioni moja hizi zitasaidia sana kupunguza michango kwa wananchi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na kuwawezesha watoto kuwa na mazingira bora ya kujifunzia” alisema Mheshimiwa Waitara.
Akiwa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, Mheshimiwa Mzee ametembelea Shule ya Sekondari ya Bomani, Shule ya Sekondari ya Ikoro na Shule ya Sekondari ya Magena na kuiagiza Halmashauri hiyo kurekebisha baadhi ya mapungufu aliyoyaona na kukamilisha ujenzi wa vyoo katika Sekondari za Ikoro na Magena.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mheshimiwa Mzee ametembelea shule mbili zinazojengwa na Serikali kupitia mradi wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP) ambazo ni Shule ya Sekondari ya Bukira na Shule ya Sekondari ya Nyasaricho.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kamati ya Usalama ya Tarime, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Elimu, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Miundombinu, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Mipango na Uratibu , menejimenti za Halmashauri ya Tarime Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Wengine walioshiriki ziara hiyo ni mwakilishi wa Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tarime, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Katibu wa Mbunge wa jimbo la Tarime Mjini, madiwani na watendaji wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa