RC APOKEA MAAFISA WA ISRAEL
Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee leo tarehe 24 Agosti, 2022 amewapokea maafisa wanne kutoka Tel Aviv Sourasky Medical Center, Lis Maternity and Women’s Hospital kutoka nchini Israel ambao wamekuja kwa ajili ya kuanzisha mradi mpya wenye lengo la kuboresha huduma za afya ya uzazi katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza baada ya kuwapokea maafisa hao, Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa amefurahi sana kwa nchi ya Israel kuanzisha mradi wa kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Mara na kuwaahidi wataalamu hao kuwa Mkoa wa Mara utawapa ushirikiano katika kutelekeza mradi huo.
Katika Mapokezi hayo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu, wataalamu wa afya na baadhi ya maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Maafisa waliopokelewa kutoka Israel ni Dkt. Gilard Rattan Moshe, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akina Mama, Binat Sessan, Muuguzi Mkunga na Mkuu wa Wodi ya Wazazi, Rinat Segal, Muuguzi Mkunga na Mkuu wa Mafunzo na Revital Levi Ari, Muuguzi Mkunga na Mkuu wa Kitengo cha Tiba Mbadala wa hospitali ya Tel Aviv.
Aidha, maafisa hao wamewasilisha nyaraka za msaada wa vifaa tiba mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani 13,500 ambayo Serikali ya Israeli imetoa kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara.
Wakizungumza wakati wa kupokea taarifa ya sekta ya afya ya Mkoa wa Mara, maafisa hao kutoka Israel wameahidi kuendelea kutoa msaada wa vifaa tiba na mafunzo ya muda mfupi kwa madaktari wa kawaida ili waweze kufanya vizuri operesheni za uzazi katika maeneo yao.
“Katika nchi nyingi zilizoendelea madaktari wa kawaida hawaruhusiwi kuwafanyia operesheni kwa akina mama wajawazito, lakini huku kutokana na upungufu wa madaktari bingwa, madaktari wa kawaida ambao hawana utaalamu na masuala ya uzazi wanaruhusiwa kuwafanyia upasuaji wajawazito jambo ambalo linaweza kuwa ni hatari” walisema wataalamu hao.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya Dkt. Juma Mfanga amewashukuru wageni hao kwa kutaka kuanzisha mradi katika Mkoa wa Mara na kuwasilisha nyaraka za msaada huo na kuwaahidi Mkoa wa Mara utawapa ushirikiano wa kutosha katika kuimarisha ushirikiano baina ya Israeli na Tanzania.
Mbali na kuembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, wataalamu hao pia wametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara katika eneo la Kwangwa na vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara.
Kabla ya kuja Mkoa wa Mara, wataalamu hao walikutana na Mganga Mkuu wa Serikali kutoka Wizara ya Afya, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya na Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa