Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amepokea kombe la ushindi la mabingwa wa CRDB Taifa Cup, Timu ya Mpira wa Kikapu Wanawake Mkoa wa Mara walioshinda katika mashindano yaliyofanyika tarehe 07-18 Juni, 2024 katika uwanja wa Chinangali, Dodoma.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo Mhe. Mtambi amesema amepokea kombe la ushindi katika mashindano ambayo vijana wa Mkoa wa Mara walishiriki na kushinda kwa kishindo.
“Sisi watu wa Mara ni wakali kama kichuri, kwenye michezo timu inayojisogeza kucheza na timu za Mkoa wa Mara tunawapiga kichuri bila nyama na tuendelee na dozi hiyo hiyo…. tuwapige kichuri bila nyama” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amempongeza Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara Mhe. Esther Matiko ambaye alikuwa mfadhili mkuu wa timu hiyo na wadau wengine wote wa michezo ambao walichangia na kuhakikisha timu ya Mkoa wa Mara inafanya vizuri katika mashindano hayo.
Mhe. Mtambi ametoa rai kwa wananchi, na wadau wote wa michezo katika Mkoa wa Mara kwa maana ya taasisi na watu binafsi na waheshimiwa wabunge wa Mkoa wa Mara washiriki katika kuchangia na kuhamasisha michezo, Mkoa wa Mara una vipaji vingi sana.
Mhe. Mtambi ameahidi kuliweka kombe hilo ofisini kwake na kila mgeni atakayefika ofisini akutane nalo ili kuonyesha uwezo wa vijana wa Mkoa wa Mara katika michezo.
Mkoa wa Mara ulifanikiwa kutwaa ubingwa wa kombe hilo baada ya kuifunga Timu ya Mkoa wa Unguja kwa mabao 74 kwa 70 na Mkoa wa Mara ukatangazwa kuwa mabingwa wa mashindano hayo.
Kwa upande wake, Mhe. Matiko amesema wamekabidhi ubingwa wa Taifa Cup inayodhaminiwa na Benki ya CRDB na yanafanyika hapa nchini kila mwaka na kwa mwaka huu Mkoa wa Mara umechukua ubingwa.
Mhe. Matiko amesema bado Mkoa una miundombinu duni sana kwa mchezo wa kikapu, kwa Manispaa ya Musoma kuna uwanja mmoja wameufufua ambao ndio ulikuwa unatumika kwenye ligi ya Mkoa na Tarime wanatumia uwanja wa Chuo cha Ualimu Tarime ambao amesema hauna hadhi.
Mhe. Matiko ameiomba Serikali na wadau kuhakikisha kuwa Mkoa unakuwa na viwanja angalau hadi ngazi ya wilaya ili kuhamasisha vijana wengi zaidi kushiriki kucheza mchezo huu wa mpira wa kikapu.
Kwa upande wake Kamishna wa Mipango na Maendeleo wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) Bwana Alloyce Renatus amesema huu ni ushindi wa kwanza na wa kihistoria kwa Mkoa wa Mara ambapo michezo yote katika mashindano hayo ilirushwa kwenye matangazo ya moja kwa moja na vyombo vya habari.
Bwana Renatus amesema Timu ya Wanawake Mkoa wa Mara ambayo inaitwa Victoria Divas ilishinda kwa ubingwa wa Taifa, nah ii imeleta heshima kwa Mkoa na kwenye ramani ya mpira wa kikapu hapa nchini, timu tishio ni Timu ya Mkoa wa Mara.
Bwana Renatus amesema timu hii pia ndio ambayo imetengeneza timu ya Fox Divas ambayo ilikuwa mshindi wa pili kwenye mashindano kwenye ligi ya Taifa na kuongeza kuwa imechaguliwa kushiriki mashindano ya kuwania kucheza Ligi ya Kikapu ya Wanawake Afrika kuanzia tarehe 28 Oktoba, 2024 hadi tarehe 2 Novemba, 2024 yatakayofanyika Zanzibar.
Bwana Renatus amesema wanatarajia timu ya Fox Divas itaenda kushindana katika mashindano hayo na ikishinda itaenda nchini Senegal kwa ajili ya kushiriki Ligi ya Afrika.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa