Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee amemuaomba Mkuu wa Majeshi Jenerali Jacob John Mkunda kuangalia uwezekano wa Jeshi la Tanzania kuwekeza zaidi katika shughuli za uzalishaji mali katika Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mzee ametoa ombi hilo wakati akimkaribisha Jenerali Mkunda aliyetembelea ofisini kwake wakati wa ziara yake ya kujitambulisha katika Vikosi vya jeshi vilivyomo katika Mkoa wa Mara na kuomba Jeshi liwekeze kwenye kilimo cha umwagiliaji na ufugaji waa samaki.
“Mkoa wa Mara tuna eneo kubwa linalopakana na Ziwa Victoria na mito lakini hamna kilimo cha umwagiliaji na hata ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba unafanywa kwa sehemu kubwa na jeshi tu, wananchi hawajapata elimu hiyo” alisema Mheshimiwa Mzee.
Amelipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kuwekeza katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba lakini ameliomba kuongeza zaidi uwekezaji na kuwafundisha wananchi wa Mkoa wa Mara kuhusiana na ufugaji wa samaki wa kitaalamu ili kuongeza uzalishaji katika Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa pamoja na mvua na uwepo wa Ziwa Victoria katika Mkoa wa Mara, hamna kilimo cha umwagiliaji na wakulima wengi hata wanaoishi kando kando ya ziwa wanalima kwa kutegemea mvua tu jambo ambalo alisema halileti tija.
“Hawa wananchi pamoja na elimu, lakini wanahitaji zaidi mfano waone jinsi kilimo cha umwagiliaji kinavyofayika na watapata nafasi ya kuiga jambo ambalo linaweza kukuza uchumi wao mmoja mmoja na Mkoa kwa ujumla” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameliomba Jeshi kusaidia katika kukabiliana na uvamizi wa wavuvi katika Ziwa Victoria unaofanywa na wavamizi kutoka nchi Jirani za Kenya na Uganda jambo ambalo amesema linahatarisha maisha na kuwapa umaskini wavuvi wa Tanzania.
Kwa upande wake Jenerali Mkunda ameshukuru kwa mapokezi mazuri aliyoyapata na kuahidi kuangalia uwezekano wa Jeshi kuwekeza zaidi katika Mkoa wa Mara.
Jenerali Mkunda amemtaka Mkuu wa Mkoa kumtumia Mkuu wa Brigedi ya Magharibi yenye Makao Makuu yake katika Mkoa wa Tabora kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo inayohitaji kufanywa na Jeshi katika Mkoa wa Mara.
Mkuu wa Majeshi amemahidi kuwa Jeshi litaendelea kulifuatilia kwa ukaribu tatizo la uvamizi wa wavuvi katika Ziwa Victoria ili kuweza kuchukua hatua stahiki kukomesha vitendo hivyo.
Aidha, amempongeza Mheshimiwa Mzee na viongozi wote wa Mkoa wa Mara kwa jitihada zinazoendelea kuchukuliwa kukabiliana na mila potofu ya ukeketaji wa wanawake katika Mkoa wa Mara.
Hii ni mara ya kwanza Jenerali Mkunda kutembelea Mkoa wa Mara tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Majeshi ya Tanzania Juni, 2022.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa