Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi katika kuboresha utendaji wa Halmashauri za Mkoa wa Mara amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kuwaondoa katika nafasi zao na kuwapangia majukumu mengine watumishi wanne wa Halmashauri ya Tarime.
Akizungumza katika kikao cha kusikiliza kero za wananchi na wafanyabiashara wa Kituo cha Forodha cha Sirari, Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa watumishi hao wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali na wanatakiwa wahamishwe kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo.
Amewataja watumishi hao kuwa ni Bwana Mawene Daniel Mangweha Afisa Hesabu Mwandamizi; Bi Mbuke Majura Makanyaga Afisa Biashara Mwandamizi, Bwana Iddi M. Baruma Afisa Ugavi Daraja la II na Bwana Alex William Ifunya Afisa Sheria Mwandamizi.
“Hawa ninataka uwaondoe Tarime mara moja ili kupisha uchunguzi wa tuhuma wanazotuhumiwa kuzifanya katika Halmashauri hii” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa pia ameliagiza Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya kumkamata na kumfungulia mashtaka Mtendaji wa Kata ya Sirari Bwana Wankuru Waryuba Mirumbe kwa tuhuma za kula fedha za mapato ya ndani “pesa mbichi” alizokasimiwa kuzikusanya na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa elimu ya kodi kwa wananchi mara kwa mara ili kupunguza magendo yanayosababishwa na wananchi kukosa uelewa wa namna ya kupitisha bidhaa zao.
“Ninawataka TRA tutumie hii nguvu tuliyoiweka kwenye kuzuia magendo hapa Sirari katika kuwaelimisha wananchi na wafanyabiashara ili waweze kupitisha bidhaa zao katika kituo hiki kwa kufuata utaratibu bila kusumbuliwa” alisema Mheshimiwa Hapi.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa ametoa zawadi ya shilingi 500,000 kwa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Sirari SSP Festo Ukulele baada ya wananchi kumsifia hadharani kuwa anafanyakazi nzuri ya kushughulikia vitendo vya uhalifu katika eneo la Sirari tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali.
Awali, wakizungumza na Mkuu wa Mkoa wananchi walimlalamikia Mtendaji wa Kata ya Sirari kwa kuwatoza wafanyabiashara kodi ya vibanda vya biashara bila kuwakatia risiti au kuwapa risiti feki ambazo hazitambuliki na kusababisha wafanyabiashara kudaiwa tena na Halmashauri wakati wameshalipa.
Akijibu tuhuma hizo, Mwekahazina wa Halmashauri ya Tarime Vijijini ameeleza kuwa Halmashauri ilipokea malalamiko hayo na walifuatilia katika mfumo wa makusanyo na kugundua kuwa Bwana Mirumbe alikuwa amekusanya zaidi ya shilingi milioni 5 ambazo hajazipeleka benki na akapewa muda wa siku saba kurejesha fedha hizo.
Wananchi pia walilalamikia kutozwa kodi kubwa wakati wa kupitisha bidhaa zao katika Kituo cha Forodha Sirari hata hivyo baada ya ufafanuzi iligundulika kuwa wananchi walikuwa wanahitaji elimu juu ya taratibu za kupitisha bidhaa zao katika mpaka huo.
Mkutano huo umehudhuliwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mheshimiwa Juma Chikoka, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Bwana Benjamin Oganga, wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Tarime, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ya Tarime na Mji wa Tarime na viongozi wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa