Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Ally Hapi ametoa saa 48 kwa mkandarasi anayejenga Uwanja wa Ndege Musoma kufika ofisini kwake kutoa maelezo kwa nini maelekezo aliyoyatoa kuhusiana na ujenzi wa uwanja huo hayajatekelezwa.
Mheshiwa Hapi ametoa maagizo hayo leo katika kikao cha wakandarasi wanaotekeleza miradi yao katika Mkoa wa Mara kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Ninatoa saa 48 huyo mkandarasi afike kutoa maelezo kwa nini maelekezo niliyoyatoa mwezi Machi, 2022 hayajafanyiwa kazi mpaka sasa na mradi bado upo nyuma sana katika utekelezaji wake” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amefikia hatua hiyo baada ya mwakilishi wa Mkandarasi huyo Beijing Construction Engineering Group (BCEG) kushindwa kutoa maelezo kwa nini maagizo ya Mkuu wa Mkoa aiyoyatoa hayajatekelezwa.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mara akiwa ameambatana na wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mara walitembelea mradi huo tarehe 1 Machi, 2022 na kukagua maendeleo ya ujenzi pamoja na kupatiwa taarifa.
Akiwa katika mradi huo, Mkuu wa Mkoa aliwagiza mkandarasi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa mujibu wa mkataba tarehe 30 Desemba, 2022 ili ndege za abiria ziweze kuanza kutua katika uwanja huo.
Mheshimiwa Hapi alimwagiza mkandarasi kufunga taa na kufanyakazi kwa saa 24, kuongeza vifaa na watumishi katika utekelezaji wa mradi huo, hata hivyo maagizo hayo hayajatekelezwa na mwakilishi wa mkandarasi alisema haiwezekani mradi huo kukamilika kwa muda uliobakia.
Maelezo ya Meneja wa Wakala Barabara (TANROADS) ambao ndio wasimamizi wa mradi huo, kwa sasa mradi huo upo katika asilimia 18 wakati muda wa utekelezaji wa mradi umeshafika asilimia 52.
Aidha mkandarasi ameshalipwa malipo ya awali na kwa sasa hana madai ya malipo ambayo ameshayawasilisha kwa TANROADS.
Uwanja wa Ndege wa Musoma ni muhimu katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Mara na kurahisisha safari za watalii wanaoingia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kukwama kwa ukamilishaji wa uwanja huu kunaathiri uchumi wa Mkoa na wananchi wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa