Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 13 Oktoba 2021 amekataa gharama za mradi wa ujenzi wa jengo la kupumzikia abiria linalojengwa katika Kivuko cha Mwigobero katika Manispaa ya Musoma unaotekelezwa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).
Akizungumza baada ya kukagua na kupokea taarifa za ujenzi wa mradi huo, Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa gharama zinazotarajiwa kutumika katika mradi huo ni kubwa na haziendani na mradi wenyewe.
“Haiwezekani mradi huu hapa ambao ukubwa wake ni sawa na darasa moja utumie shilingi milioni 86, mimi kama Mkuu wa Mkoa nemeukataa mpaka hapo nitakapopata maelezo ya kuridhisha kuhusu gharama hizi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Hata hivyo Mheshimiwa Hapi ameipongeza TEMESA kwa kutekeleza kwa haraka maagizo yake aliyoyatoa mwezi Mei mwaka huu akiwa katika ziara kukagua miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Musoma.
“Kutekeleza maagizo yangu ni jambo moja, kutekeleza kwa ukweli, uaminifu na uadilifu ni jambo jingine, sikubaliani na gharama hizi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Amemtaka Kaimu Meneja wa TEMESA kuwasilisha michoro na makadirio haliso ya gharama za ujenzi huo ofisini kwake ili kujiridhisha na gharama hizo za mradi.
Awali, akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Kaimu Meneja wa TEMESA Mkoa wa Mara Bwana Vitalis Bilauri ameeleza kuwa mradi huo utajenga jengo ambalo litakuwa na matundu manne ya vyoo, ofisi moja, sehemu ya kukatia tiketi na sehemu ya kupumzika abiria.
Ameeleza kuwa michoro na makadirio halisi ya mradi huo bado havijaletwa kutoka TEMESA Makao Makuu lakini wamepokea mchoro wa awali, mkandarasi wa mradi huo na maelekezo ya kuanza kwa ujenzi huo.
Kwa upande wake, Bwana Christopher Antony, dereva wa pikipiki katika eneo hilo amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutoa maelekezo na kuyafuatilia kuona utekelezaji wake.
“Mheshimiwa usingefika hapa usingejua gharama hii wanayotaka kutumia hapa kwenye huu mradi, jengo hili ni dogo sana ukilinganisha na gharama wanayosema itatumika” alisema Bwana Antony.
Aidha Bwana Antony amewataka watendaji kufanya kazi kwa uadilifu ili kulinda fedha za umma zinazotumika kwenye miradi.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dokta Alfany Haule na watendaji wa TEMESA na viongozi wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa